Home » » BUNGE LA KATIBA LIAHIRISHWWE,TWENDE KWENYE KURA YA MAONI

BUNGE LA KATIBA LIAHIRISHWWE,TWENDE KWENYE KURA YA MAONI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Bunge Maalumu la Katiba linatarajiwa kuanza mnamo Agosti 5 mwaka huu, likiendeleza mjadala wa siku 70 wa rasimu ya Katiba.
Bunge hilo liliahirishwa Aprili 25 ili kupisha Bunge la Bajeti lililoisha hivi karibuni.
Kabla hata halijaahirishwa, tayari hali ilishachafuka baada ya wajumbe wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutoka nje ya ukumbi wa Bunge wakilalamikia pamoja na mambo mengine kupindishwa kwa rasimu ya Katiba.
Kikubwa wanachopigia kelele Ukawa ni kuheshimiwa kwa rasimu ya Katiba hasa suala la muundo wa Serikali ya Muungano.
Tangu Bunge hilo lilipoanza vikao vyake Februari 26 mwaka huu, mjadala umejikita kwenye muundo wa Serikali ambapo Ukawa wanataka muundo wa Serikali tatu uliopendekezwa na rasimu ya Katiba, huku CCM wakisisitiza serikali mbili.
Kutokana na tofauti hiyo, wajumbe wa Ukawa wameapa kutorudi Bungeni ifikapo Agosti 5, huku kukiwa na juhudi nyingi za kuwashawishi kurudi ikiwamo ya Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta kuitisha vikao vya kutafuta suluhu.
Hadi sasa haijajulikana kuwa Bunge hilo litafanyikaje ikiwa wajumbe wa Ukawa zaidi ya 200 wataendelea na mgomo wao.
Lakini kwa kuwa kinachogombewa kikubwa ni muundo wa Serikali, huku CCM wakilalamikia utendaji wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba, katika ukusanyaji wa maoni, nadhani suluhisho ni kurudi kwa wananchi.
Turudi kwa wananchi na kuwapa fursa nyingine ya kuamua upi hasa muundo wa serikali wanaoutaka, wa serikali mbili, tatu au moja.
Tume ya Jaji Warioba ilizunguka karibu nchi nzima ikihoji wananchi, kisha ikayachambua maoni na kutengeneza rasimu ya kwanza na ya pili zote zikionyesha muundo wa Serikali tatu.
Sasa CCM wanaona kiama chao kimefika, wanataka kupeleka puta mchakato huo ili waendelee na Serikali zao mbili.
Pamoja na kwamba kutakuwa na kura ya maoni baada ya Bunge hilo, nadhani suluhisho kwa sasa ni kupiga kura ya awali ya maoni ili kuamua tu mfumo wa Serikali.
Kura hii ikishapigwa na wananchi wakiamua muundo huo, basi wajumbe warudi Bungeni waendelee kujadili vipengele vya rasimu.
Kwanza kura ya maoni kuhusu muungano, ilipaswa kupigwa kabla hata mchakato wa Katiba haujaanzishwa. Hiyo ingeondoa dukuduku la muda mrefu kutoka kwa wananchi kuhusu muundo wa muungano.
Muungano wenyewe una maswali mengi yasiyo na majibu hadi leo kwa kuwa haukushirikisha wananchi tangu awali.
Hii ingekuwa fursa maalumu ya kuwashirikisha wananchi kwa kupiga kura ya maoni ya kama wanautaka muungano na uwe wa Serikali ngapi.
Kwa hali ya sasa, hata Ukawa wakirudi Bungeni, wataishia kutukanana na wajumbe wa CCM hadi siku 70 zitakwisha. Pesa za walipa kodi zitaliwa bure na tusipate Katiba tunayoitaka.
Bora mchakato huo urudishwe kwa wananchi watoe suluhusho
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa