Home » » DARASA HURU: HATA KAMA UMBEA UNASAIDIA KUONDOA ‘STRESS’ BASI TUTETE KWA STAHA

DARASA HURU: HATA KAMA UMBEA UNASAIDIA KUONDOA ‘STRESS’ BASI TUTETE KWA STAHA

Salamu zangu kwenu wapenzi wa darasa huru. Ni juma jingine tena tunakutana kufahamishana mambo yanayogusa maisha yetu ya kila siku, lengo ikiwa ni kuelimishana, kuhabarishana na kusaidiana katika kuwekana sawa ili maisha yasonge vyema.
Kwa wale ambao wamekumbwa na changamoto mbalimbali za maisha zilizowalazimu kusimamisha shughuli zao za kujitafutia riziki za kila siku, nawapa pole. Nawaombea kwa Mungu awape nafuu na warejee katika pilikapilika za utafutaji maisha na kuingiza riziki hata kama ni kidogo, hasa mwezi huu wa kwanza ambao kwa jinsi mambo yalivyo mengi, unaweza kutamani ardhi ipasuke uingie.
Tuachana na hilo, turejee katika mada yetu ya leo ambayo najua inatugusa wengi wetu kwani suala la umbea ni kama jambo la kawaida kwa baadhi ya watu. Wao bila umbea wanaona kama kuna kitu wamekosa. Kwao umbea ni jambo la kawaida hawaoni haya kusengenya.
Zamani nilikuwa naona kama watu wa namna hiyo hawajastaarabika. Kifupi nilikuwa nawaona kama watu wa ajabu. Lakini baada ya kusoma majarida mbalimbali na kugundua kuwa moja ya njia ya kupunguza msongo wa mawazo ni umbea, nikaanza kuelewa.
Mbali na kusoma majarida hayo, mwaka jana kuna utafiti ulifanywa ukabainisha kuwa umbea unasaidia kupunguza msongo wa mawazo. Kutokana na hilo ni dhahiri kuwa suala la umbea ni zuri katika maisha yetu ya kila siku. Tunawashukuru watafiti hao kwa kuwafungua watu kama mimi niliyekuwa na mawazo hasi juu ya umbea.
Kwa mfano, unaweza ukawa umekaa na mambo mengi yanakusumbua kichwani, mara akaja swahiba wako akakupa umbea, ukafurahi hata ukasahau yale uliyokuwa unawaza kwa muda.
Lakini kuna mambo ambayo watu wengi tunakosea kuhusu umbea. Unaweza kukuta mtu anamzungumzia mtu fulani kwa mwenzake au kundi la watu, lakini nusu ya maongezi yale yanakuwa siyo ya kweli. Mambo ya uongo ndiyo yanakuwa mengi. Yaani kama ni wewe ulikuwa unazungumziwa halafu mtu akaja kukueleza kuwa watu fulani walikuwa wanakuzungumzia hivi na hivi, lazima utashikwa na butwaa.
Utajiuliza maswali mengi yasiyokuwa na majibu. Ni kwa nini watu wanazungumza uongo kiasi hicho? Hata kama ni umbea basi wazingatie na ukweli. Iweje ukweli wauache, halafu waseme uongo mtupu? Sasa huo sijui huo tuuite umbea au uzushi.
Mbaya zaidi mambo kama hayo yanaweza kusambaa na kumharibia mtu sifa kutokana na watu wachache wasiokuwa na busara. Mtu anajiropokea tu mambo yasiyo ya kweli hadi unashangaa kama ametumwa au labda umemkosea, kumbe hakuna kitu. Tena ukikutana naye, anakuchekea na kukusalimia kwa furaha zote.
Kuna mambo wakifanya watoto wadogo unaweza kuelewa kutokana na umri wao, lakini wakifanya watu wazima wenye akili ni jambo la kushangaza kwa kweli. Tujaribu kuwa na staha jamani hata kama tunateta basi tujaribu kuwa wakweli. Mbonatunaacha mambo mazuri, tunasema mabaya tu. Tuseme yote kwa usawa tukizingatia ukweli kwani umbea hauepukiki katika maisha yetu.
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa