Home » » DC AONYA WANAUME KUTUMIA MAVUNO KUONGEZA WAKE.

DC AONYA WANAUME KUTUMIA MAVUNO KUONGEZA WAKE.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MKUU wa Wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro amewaonya wanaume hususani wa maeneo ya vijijini ambao hupenda kuongeza wake kipindi cha mavuno sababu ya kuchezea chakula na kusababisha baa la njaa kuingia kwenye familia zao, kitendo ambacho amepiga marufuku.
Matiro alitoa onyo hilo kutokana na kuwepo kwa tabia hiyo ya baadhi ya wanaume ambao hupenda kuongeza wake wengi pale wanapopata mavuno mengi, na kusahau kuhifadhi chakula cha kujikimu na pale msimu wa kilimo unaporejea, huanza kuomba msaada serikalini.
Akizungumza juzi kwenye mikutano mitatu ya hadhara kwa nyakati tofauti na wanakijiji cha Itwangi, Didia na Imesela katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Matiro alisema kutokana na mwaka huu kuwa na neema ya chakula, mwananchi au kijiji kitakachochezea chakula serikali haitapeleka msaada kwao.
Kwa upande wake, Ofisa Kilimo wa Kijiji cha Ilola, Tarafa ya Itwangi, Hazina Thomasi aliishauri serikali itunge sheria ndogo ambayo itawabana wanaume wanaopenda kuuza chakula chote nyumbani kwake, na kuzitumia fedha kwa matumizi yasiyo rasmi ikiwamo kuoa ovyo na kunywea pombe.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Kiomoni Kibamba alisisitiza wananchi hao kuacha tabia ya kuendekeza kulima mazao ya muda mrefu ambayo ni bahati kuhimili ardhi ya Shinyanga, bali wawe wanalima vyakula vya muda mfupi ambao ni mtama, choroko, viazi vitamu angalau hata ekari moja moja.
Baadhi ya wananchi wa Kata ya Imesela, Hadija Kashindye na James Kulwa walikiri kuwapo tabia hiyo katika baadhi ya familia wanapopata mavuno mengi wanaume husahau shida ya chakula na kuuza kwa kuongeza familia nyingine.
 CHANZO : HABARI LEO.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa