Home » » 'Msiozeshe watoto kwa tamaa ya mifugo'

'Msiozeshe watoto kwa tamaa ya mifugo'

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

OFISA Elimu mkoani Shinyanga, Mohamed Kahundi, amewashauri wazazi kusomesha watoto wao na si kuwakatisha masomo kwa ajili ya kuwaozesha ili wapate mifugo, kwakuwa kufanya hivyo kunawanyima haki ya kupata elimu na kuwajengea umasikini.
Alitoa ushauri huo mwishoni mwa wiki kwenye mahafali ya kidato cha nne katika shule ya sekondari Kom. Ushauri huo ulitokana na kuendelea kuwepo kwa wazazi wanaokataa kusomesha watoto wao wa kike ili wawaozeshe na kupata mifugo.
Kahundi alisema kwenye dunia ya sasa elimu ndio kila kitu katika kumjenga mtoto kimaisha, hivyo ni vyema wazazi mkoani Shinyanga wakabadili mitazamo yao hasi na kujikita kuwekeza elimu kwa watoto wao watakaokuja kuwasaidia kimaisha baadaye.
"Ukisomesha mtoto ni sawa na kujiwekea hazina yako ya baadaye pale utakapozeeka na kuishiwa nguvu za kufanya kazi, kwa sababu yeye ndiye atakayekuja kugeuka kuwa mlezi wako na atakulea vizuri akiwa na elimu,” alisema.
Aidha, aliongeza kuwa ni vyema sasa wazazi mkoani humu wakaacha kuthamini mifugo kuliko utu wa mtu, bali wapende elimu na kusomesha watoto wao ili hapo baadaye waje wale matunda ya elimu na kuwa na maisha bora na kutokomeza umasikini.
Mwenyekiti wa Bodi ya shule hiyo, Peter Kuguru, aliwataka wazazi kujenga utamaduni wa kufuatilia maendeleo ya watoto wao shuleni na kuwatimizia mahitaji yote, ili kuwaepusha na vishawishi ambavyo vimekuwa vikikatisha ndoto zao.
Mkuu wa shule hiyo, Mwita Warioba alisema wanafunzi waliohitimu masomo hayo ya kidato cha nne ni 144, wasichana wakiwa 60 na wavulana 84.
CHANZO GAZETI LA HABARI LEO

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa