Home » » MBUNGE AZZA HILAL AWAHIMIZA AKINA MAMA KUWEKEZA KATIKA ELIMU BORA KWA WATOTO WA KIKE

MBUNGE AZZA HILAL AWAHIMIZA AKINA MAMA KUWEKEZA KATIKA ELIMU BORA KWA WATOTO WA KIKE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mbunge wa viti Maalum mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Azza Hilal (CCM) amewataka akina mama kujitahidi kuwekeza katika elimu kwa watoto hususani watoto wa kike na kuwa mstari wa mbele kuhakikisha watoto wa kike wanapata elimu bora.
Mheshimiwa Azza Hilal (pichani) ameyasema hayo leo Jumatano Septemba 20,2017 katika ukumbi wa Mountain View Hotel uliopo katika kata Tinde wilaya ya Shinyanga wakati akifungua Mafunzo ya ujasiriamali,fedha na mikopo kwa akina mama yaliyoandaliwa na Benki ya CRDB tawi la Shinyanga.
Mbali na kuwaasa akina mama kutumia vyema mikopo wanayopata kuitumia kwa malengo waliyokusudia,pia aliwakumbusha kuwekeza kwa watoto wao.
Alisema mkoa wa Shinyanga ni miongoni mwa mikoa inayoongoza nchini kwa kuwa na takwimu kubwa (asilimia 59) ya mimba za utotoni na ndoa za utotoni hivyo jitihada mbalimbali za pamoja zinahitajika ili kuondoa vitendo hivyo ambavyo vinawanyika haki watoto wa kike kuendelea na masomo yao. 
“Nitumie fursa hii kuwakumbusha kuwa sisi akina mama kuwa tuna wajibu mkubwa kuhakikisha watoto wetu wa kike wanapata elimu iliyo bora,kuhakikisha pia watoto ambao hawakupata fursa ya kufaulu mtihani wa darasa la saba ili kuendelea na masomo ya kidato cha kwanza tunawatafutia njia mbadala ya kuweza kujikomboa na maisha badala ya kukimbilia kuwaozesha”,alieleza Hilal.
“Kumekuwa na tabia, mtoto akiingia darasa la saba anaambiwa na wazazi wake kuwa akafanye vibaya kwenye mtihani,naomba tuanze sisi akina mama kukataa,kwanini unakubali mtoto wako aambiwe na baba yake kuwa akafeli mtihani?”,alihoji mbunge huyo.
Aidha alisema ili kuondoka kwenye takwimu za kuitwa watu ambao hawajasoma ni vyema akina mama wakawa mstari wa mbele katika kupigania haki za watoto.
“Wenye kulibeba hili ni akina mama kwa sababu akina baba tunajua wametanguliza pesa mbele,najua hakuna ambacho mwanamke anaweza akaamua kukifanya na kikashindikana,naomba tuanze kuwapatia watoto malezi ya kupenda elimu na kuepuka vishawishi wakiwa wadogo”,alisema Hilal.
“Niwaombe sana tuwe karibu na watoto wetu wa kike, ili waweze kukushirikisha kwa jambo lolote watakalokutana nalo,usipokuwa karibu na mtoto wako,hata kama atabakwa hawezi kujibu kwako,lakini kama umejenga utamaduni wa kuongea naye kama rafiki yako,kama ndugu yako wa karibu hawezi kusita kukwambia jambo lolote zuri ama baya litakalokuwa limemtokea”,alieleza Mhe. Hilal.
Mbunge huyo pia alieleza kusikitishwa na vitendo vya baadhi ya wazazi kuficha matukio ya watoto wanapofanyiwa vitendo vya kikatili kwa watoto wa kike.
“Watoto wengi wa kike wanafanyiwa vitendo vya kikatili ikiwemo kubakwa,kwa taarifa nilizopewa polisi wazazi mnaficha vitendo vya kikatili dhidi ya watoto,kwanini mnaficha vitendo hivi viovu? Mtoto anafanyiwa vitendo vibaya halafu mzazi unaficha?,inakusaidia nini?,ni bora ukakubali fedheha ya siku moja lakini haki ya mtoto wako ikapatikana”,alisema.
“Inasikitisha sana pale mnapoitwa kutoa ushahidi wa kesi za ukatili dhidi ya watoto halafu mnakataa,kwa kweli hamuwatendei haki watoto wetu,Kama mzazi unatetea uovu wa namna hii wewe ni muuaji kwa sababu wewe mzazi usipotoa ushirikiano hatma ya kesi haitakuwepo matokeo yake mtabaki kulalamika tu kuwa watuhumiwa mnawapeleka polisi lakini mnawaona wapo tu mtaani,sasa mtuhumiwa ataachaje kuwepo wakati hutoi ushirikiano?”,aliongeza Mhe. Hilal.
Aidha aliwataka wadua wote wa haki za watoto kuendelea kulaani vitendo vya ukatili dhidi ya watoto huku akiwasisitiza wazazi na walezi watoto kutofumbia macho vitendo na kumaliza kesi kienyeji kwani haki za watoto zinapotea.
Katika hatua nyingine kutokana na maendeleo katika sayansi na teknolojia aliwatahadhalisha wazazi na walezi kuwa makini na matumizi ya mitandao kwani baadhi ya watoto hususani wanaosoma katika shule zenye mabweni ‘Boarding’ wanafanya michezo mibaya kutokana na mambo wanayoyaona mitandaoni.
Mbunge huyo aliishukuru Benki ya CRDB kkutoa elimu kuhusu masuala ya fedha na mikopo elimu ambayo itawasaidia wananchi kuendesha biashara zao vizuri.
Hata hivyo Meneja wa Benki ya CRDB alisema benki hiyo itaendelea kufungua matawi katika maeneo mbalimbali ya vijijini na kuwapatia elimu wajasiriamali waliopo kwenye vikundi mbalimbali.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa