Home » » Wakulima walilia matrekta makubwa

Wakulima walilia matrekta makubwa

Wakulima wa Kijiji cha Ngulu Kata ya Ngogwa wilayani Kahama mkoani Shinyanga wameiomba Serikali kuwasaidia kupata matrekta makubwa mawili yatakayowasaidia kuboresha kilimo chao cha zao la mpunga.
Wakizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kijiji hicho juzi kuangalia utekelezaji wa miradi ya maendeleo wakulima hao walisema pamoja na kupatiwa msaada wa matrekta madogo mawili aina ya power tiller hitaji lao kwa sasa ni trekta kubwa lenye uwezo tofauti na hayo madogo.
Walisema matrekta madogo waliyonayo hayana uwezo wa kulima eneo kubwa na kwamba iwapo watapatiwa msaada wa makubwa kupitia mpango wa Kilimo Kwanza wanaamini wengi wao wataongeza maeneo yao ya kilimo na hivyo kujiongezea kipato kutokana na mazao watakayopata.
"Kijiji chetu kina ardhi ya kutosha kwa ajili ya kilimo, tatizo linalosababisha tushindwe kuongeza maeneo ya kilimo ni kutokuwa na pembejeo za kisasa, tulipewa power tiller mbili, lakini kwa kweli uwezo wake ni mdogo, tunashauri tupatiwe trekta kubwa mbili, hizi zitamudu," alieleza Naomi Malando Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Ngulu.
Hata hivyo, mmoja wa wakulima katika kijiji hicho aliishauri Serikali iwe makini wakati inapotoa kazi kwa mawakala wanaosambaza pembejeo za kilimo kutokana na baadhi yao kutokuwa waaminifu wenye tabia ya kuwasambazia wakulima pembejeo zisizo na ubora.
"Tunaiomba Serikali iwe makini kwa mawakala wanaopewa kazi ya kusambaza pembejeo za kilimo kwa wakulima, wengi siyo waaminifu, wanatumia nafasi wanayopata kuwanyonya wakulima wakijali zaidi kupata faida kubwa, sasa hii ni hasara kwetu, mwaka jana walichelewa kugawa pembejeo kwa wakati."
"Kibaya zaidi hata mbegu wanazotuuzia hazina ubora, mavuno yake ni kidogo ikilinganishwa na mbegu tulizozizoea, mbegu ya mpunga kwa msimu uliopita haikuwa nzuri na hata upande wa mahindi ni hivyo hivyo, wakala alifanya ujanja akijali zaidi faida, sasa tunaomba hawa watu wamulikwe, waache kutuchumia," alisema Mahega Fundi.
Katika hatua nyingine wakazi wa kijiji hicho wameupongeza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kahama kwa kuwajengea ghala la kisasa la kuhifadhia mazao hali ambayo imewapunguzia kero ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya maghala ya kukodi mjini Kahama.
"Tunaishukuru halmashauri kutujengea ghala la kisasa kupitia mradi wa DASIP, limetusaidia sana, maana hapa tuna mazao mengi kila kipindi cha mavuno tulikuwa tukipata shida ya kupata eneo la kuyahifadhi, ghala lililokuwepo lilijengwa kienyeji halikuwa na nafasi za kutosha, sasa kero hiyo haipo tena," alisema Naomi Malando

Chanzo;Majira

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa