Na
Mwandishi Wetu, Kahama
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Shinyanga,
kimesema kelele zinazopigwa na wapinzani katika majukwaa, kwa lengo la
kukikashifu na kukichafua chama hicho, ni sawa na dawa ya Kikombe cha Babu wa
Loliondo.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, aliyasema hayo juzi katika
uzinduzi wa kampeni za udiwani wa Kata ya Bungarama, wilayani hapa. Uchaguzi
huo unafanyika baada aliyekuwa diwani wa kata hiyo kufariki dunia.
Alisema kuwa, anavifananisha vyama hivyo na dawa ya Babu wa Loliondo, kutokana
na watu wengi kuacha kwenda hospitali kupata matibabu na hivyo kukimbilia kwa
babu huyo.
“Dawa ya Babu iliwavuta wengi bila ya kujali kuwa kulikuwa na sehemu nyingine
ya kupata matibabu, ikiwamo hospitalini. Tukio hilo ni sawa na wanaohama Chama
Cha Mapinduzi na kukimbilia upinzani, wakidhani huko watapata nafuu.
“Chama Cha Mapinduzi kwa sasa, ndio chenye dola, kwa hiyo, chuki na kashifa
zinazotolewa na vyama vingine juu ya CCM, bado haziwezi kumbadilisha mwananchi
kwenda katika upande wa pili.
“Watanzania bado wana imani na chama chao ambacho ndio kimewatoa mbali, kwa
hiyo, wana CCM lazima tushikamane kwa kuacha tofauti zetu,” alisema Mgeja.
Kwa mujibu wa Mgeja, siyo kila mwanachi anayehamia chama cha upinzani, matatizo
yake yatakwisha kwa kuwa vyama hivyo vimekuwa vikihubiri habari za chuki na
kauli za kashfa katika majukwaa.
“Nawaambia siyo kila mtu anayehamia katika chama cha upinzani, matatizo yake
yatakwisha, CCM ndiyo chama kilicho madarakani na ndiyo tumaini pekee la
Watanzania,” alisema.
Katika mkutano huo, watu 83 ambao ni wanachama wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) walirudisha kazi akiwamo ya Katibu wa Kijiji cha Buyange
ulipofanyika mkutano huo.
Uchaguzi huo unatarajia kufanyika mwishoni mwa mwezi huu, kutokana na diwani wa
kata hiyo kupitia CCM, Peter Kisiminza, kuuawa na watu wasiojulikana.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment