Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha (aliyevaa miwani)akizindua Bango la Kwanza lililoandikwa kwa Lugha ya Kiswahili linaloelezea utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa barabara ya Kahama – Bulyanhulu JCT- Kakola
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amezindua Bango la Kwanza lililoandikwa kwa lugha ya Kiswahili linaloelezea utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa barabara ya Kahama – Bulyanhulu JCT- Kakola yenye urefu wa Km 73 ikiwa ni utekelezaji wa ushauri wake wa kuanza kutumia Lugha ya Kiswahili katika Mabango yote ya miradi ndani ya Mkoa wa Shinyanga.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika leo Jumatatu Septemba 23,2024 Mhe. Macha amesema Lugha ya Kiswahili inatumiwa na wananchi wengi na kwa kuwa miradi yote ni ya wananchi hivyo wanapaswa kuelewa nini kimeandikwa na nini kinatekelezwa na Serikali katika maeneo yao.
“Nawapongeza TANROADS kutayarisha na kuweka bango hili kwenye mradi wa ujenzi wa Kilometa 73 ya Kahama hadi Kakola kwa kiwango cha Lami ukaogharimu zaidi ya shilingi Bilioni 101 .2. Hili ni bango la Kwanza kuandikwa kwa Lugha ya Kiswahili katika Mkoa wa Shinyanga. Naagiza pia kwenye maeneo mengine miradi sekta mbalimbali mabango yaandikwe kwa Lugha ya Kiswahili, hata kama mtaweka Bango la Kiingereza lakini pia muweke la Kiswahili kwani Lugha ya Kiswahili inajitosheleza kwa kila kitu”,ameeleza Mhe. Anamringi.
"Nawapongeza sana Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Shinyanga chini ya Mhandisi Samwel Joel Mwambungu kwa kuwa wa kwanza kutekeleza ushauri wangu wa kuanza kutumia Lugha ya Kiswahili katika mabango yote yanayoelezea miradi inayotekelezwa kwa wananchi ndani ya Mkoa wa Shinyanga, hongera sana Meneja Mhandisi Mwambungu," amesema Mhe. Macha.
0 comments:
Post a Comment