Home » » Teknolojia na uhalifu Wizi wa kimtandao unavyoshamiri duniani

Teknolojia na uhalifu Wizi wa kimtandao unavyoshamiri duniani

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Maendeleo ya sayansi na teknolojia yanalenga kufanya maisha ya binadamu duniani yawe rahisi zaidi.
Kumekuwapo na usemi kuwa mawasiliano ya mtandao yamewezesha dunia kuwa kama kijiji; kwa maana kwamba binadamu hahitaji tena kutumia muda mrefu kupeleka ujumbe wake kwa barua itakayotumia wiki kadhaa kumfikia mhusika.
Leo hii ipo mifumo mingi ya kuwasiliana papo kwa hapo dunia nzima kama vile barua pepe, ujumbe mfupi wa maneno, whatsup, facebook, twitter, instagram na mitandao mingine.
Wakati maendeleo hayo yakishika kasi, wahalifu nao wanafikiria jinsi ya kujipatia fedha kupitia mifumo hiyo.
Licha ya kuwepo na udhibiti wa hali ya juu, wahalifu nao wamejitahidi na mara kadhaa wamefanikiwa kwa kuingilia mifumo hiyo ya kielektroniki.
Kwa mfano, hapa nchini kumekuwepo na matukio kadhaa ya wizi wa mitandao hasa katika vyombo vya fedha zikiwamo benki.
Uchunguzi mbalimbali wa kimataifa unaonyesha kuwa wezi wamekuwa werevu kiasi kwamba huweza kutumia teknolojia kupata taarifa za siri za watumiaji wa kompyuta zilizounganishwa kwenye mitandao.
Wanatumia programu mbalimbali zinazoitwa virusi vya kompyuta kupata taarifa hizo. Virusi hao ni kama vile trojans, worms, viruses, hacktools, rootkits na adware.
Kwa kutumia virusi hao, maharamia wa wizi wa mitandaoni huweza kupata taarifa za siri zilizohifadhiwa kwenye kompyuta na mmiliki wake.
“Siku hizi kuna uhusiano wa kampuni hasa kati ya maharamia wa njia za mitandao na kampuni au vikundi vinavyojihusisha na jinai. Hawa ndio wanaojihusisha na jinai na ndio mara nyingi wanakuwa ni chanzo cha kuwezesha kusambaza mafanikio ya wizi kwa njia ya mtandao,” anasema Daniel Kamau kutoka kampuni ya inayojihusisha na utengenezaji wa kompyuta pamoja na programu zake ya Microsoft.
Wizi wa mitandao duniani
Wizi wa mitandao hauiandami Tanzania tu bali ni tatizo la dunia. Mbinu za uingiliaji wa mitandao umekuwa wa kiwango cha juu.
Ripoti ya utafiti iliyotolewa mwaka huu na Kampuni ya Kimataifa ya Teknolojia ya Mawasiliano ya Kompyuta (IDC) ikishirikiana na Chuo Kikuu cha Singapore, inaonyesha kuwa kwa mwaka huu dunia inatarajia kupoteza Dola za Marekani 500 bilioni kwa ajili ya kukabiliana na wizi wa mitandao.
“Dola nyingine 127 zitashughulikia suala la ulinzi, ikiwamo kiasi cha Dola 8 bilioni katika maeneo ya Mashariki ya Kati na Afrika,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Vile vile inaelezwa kuwa Dola 364 bilioni zitashughulikia suala la uvujaji wa taarifa za siri zinazohusu kampuni.
Wateja binafsi kote ulimwenguni wanaelezewa kwenye ripoti hiyo kwamba wanatarajiwa kutumia Dola 25 bilioni kulinda fedha zao.
“Wizi wa njia ya mtandao unahamasishwa na tamaa ya fedha. Wanachofanya ni kuchukua taarifa muhimu za mtu, kitambulisho, namba za siri au hata fedha,” anasema Mkurugenzi Mkuu Microsoft, David Finn.
Mkuu wa kitengo cha utafiti cha IDC, John Gantz anasema vitendo vya wizi wa mtandao ni hatari kwa kuwa madhara yake ni makubwa, kama vile kuangusha uchumi wa kampuni, taasisi au biashara ya mtu binafsi.
Kwa upande wake, Profesa Biplab Sikdar pia kutoka kampuni hiyo anasema utafiti unaonyesha kuwa wizi wa mitandao unazidi kuongezeka siku hadi siku duniani.
Hata hivyo, anasema nchi zinazoongoza kwa matukio hayo ni pamoja na Brazil, China, Ufaransa, Ujerumani, India, Indonesia, Japan, Mexico, Poland, Urusi, Singapore, Ukraine, Uingereza na Marekani.
Ripoti hiyo inaonyesha kompyuta nyingi zilizochunguzwa katika baadhi ya nchi hizo, zilikuwa zimefanyiwa upekuzi wa kimtandao ili kupata taarifa za siri za wamiliki.
Mbinu ya kukabili wizi
Kutokana na kuongezeka kwa vitendo hivyo, Finn anaeleza kuwa wamebuni kompyuta mpya pamoja na programu zinazoziba mianya ya wizi wa aina hiyo.
Hata hivyo, baadhi ya wataalamu duniani wanasema ipo haja ya mbinu nyingi zaidi kubuniwa ili kuzuia vitendo vya wizi.
Hii ni pamoja na uzuiaji wa utengenezaji wa ovyo wa programu za kompyuta na kuweka mifumo ya usimamiaji wa mitandao utakaowabaini wahalifu na kuwachukulia hatua.
 Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa