Home » » RAIS Jakaya Kikwete amewataka viongozi wa dini nchini, kujiepusha na tabia ya kuwakaribisha wanasiasa ambao hutumia fursa hiyo kufanya siasa katika nyumba za ibada

RAIS Jakaya Kikwete amewataka viongozi wa dini nchini, kujiepusha na tabia ya kuwakaribisha wanasiasa ambao hutumia fursa hiyo kufanya siasa katika nyumba za ibada


RAIS Jakaya Kikwete amewataka viongozi wa dini nchini, kujiepusha na tabia ya kuwakaribisha wanasiasa ambao hutumia fursa hiyo kufanya siasa katika nyumba za ibada jambo ambalo linaweza kusababisha machafuko.

Alisema wakati Taifa likielekea katika Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu ni muhimu kwa viongozi wa madhehebu ya dini nchini wakachukua tahadhari ya kuepuka kutumiwa vibaya na baadhi ya wanasiasa wanaotaka kutumia nyumba za ibada kujitafutia kura.

Rais Kikwete aliyasema hayo jana wakati akitoa salamu zake kwa waumini mbalimbali baada ya ibada ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Askofu Mpya wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga, Liberatus Sangu iliyofanyika katika Kanisa Kuu Parokia ya Mama Mwenye Huruma mjini humo.

"Tabia ya wanasiasa kupenda kutumia nyumba za ibada ili kujipigia debe inaweza kuwagawa waumini kutokana na itikadi za vyama vyao hivyo ni vyema wakazuiliwa kabisa kufanya siasa katika nyumba za ibada," alisema.

Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, alisema wakati Uchaguzi Mkuu ukikaribia, kuna baadhi ya wanasiasa wanaozunguka katika nyumba za ibada wakitaka kuungwa mkono na waumini hali inayoweza kusababisha mapigano kati yao kutokana na itikadi za vyama.

"Niwaombe viongozi wenzangu wa madhehebu ya kidini nchini, tuchukue tahadhari kubwa na hawa viongozi wa kisiasa, acheni kuwapa nafasi katika Makanisa au Misikiti ni hatari, ndani ya waumini wenu, kila mmoja ana itikadi tofauti za kisiasa.

"Msiruhusu siasa kuingia kwenye dini na dini kuingizwa katika siasa, tukiweza kuzuia hali hii tutakuwa tumefanya jambo kubwa, Makanisa na Misikiti ibaki kuwa nyumba za ibada si majukwaa ya siasa, tusaidieni katika hili," alisema Rais Kikwete.

Alisema hali ya amani na utulivu uliyopo ukitoweka, itakuwa vigumu kuirejesha hivyo ni jukumu la kila Mtanzania kuhakikisha anailinda amani iliyopo kwa gharama yoyote pamoja na viongozi wa dini ambao wanamchango mkubwa wa kudumisha amani.

Akifafanua sababu za kutoruhusu siasa katika nyumba za ibada, Rais Kikwete alisema kama chama kinachotafuta wapigakura kwenye Makanisa au Misikiti kitashindwa ni wazi dhehebu husika litakuwa limeshindwa na kusababisha machafuko makubwa miongoni mwa waumini wake.

"Viongozi wa kisiasa kwenda Kanisani au Msikitini, wakija wakaribisheni, akianza kuhubiri siasa mwambieni hapana, hapa siyo mahala pake, siasa inafanyika katika majukwaa hapakufai, nenda huko mkashindane kwa hoja, hapa tunahubiri neno la Mungu," alisema.

Akizungumzia mauaji ya kikatili ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albinism) na wanawake vikongwe kutokana na imani za kishirikina, aliwaomba viongozi wa dini kuongeza juhudi za kukemea mauaji hayo ambayo yanalitia doa Taifa.

Aliwaomba viongozi wa dini kuwaelimisha waumini wao juu ya ubaya wa kutoa roho za watu wasio na hatia kwa sababu ya kuendekeza imani potofu za kishirikina zisizo na ukweli.

"Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi, madhehebu yote ya dini na itakuwa tayari kutoa msaada wake pale itakapohitajika kufanya hivyo ili kuiwezesha Tanzania kuwa mahali pa amani, upendo, mshikamano na utulivu," alisema.

Kwa upande wake, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcius Ngaralekumtwa, alimpongeza Askofu Sangu kuwa Askofu wa jimbo ambalo halikuwa na kiongozi kwa kipindi cha miaka mitatu kutokana na kifo cha aliyekuwa Askofu wake Hayati Mhashamu Aloysius Balina aliyefariki dunia Novemba, 2012.

Ibada hiyo pia ilihudhuriwa na Maaskofu mbalimbali nchini wakiongozwa na Askofu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, viongozi wa kisiasa.

Chanzo Gazeti la Mwananchi.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa