Home » » WANANCHI MAGALATA WATAKIWA KUJIUGA NSSF

WANANCHI MAGALATA WATAKIWA KUJIUGA NSSF

Na Editha Edward, Shinyanga
WANANCHI wa Kijiji cha Magalata kilichopo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, wametakiwa kujiunga na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii, NSSF.

Akizungumza mjini hapa jana, Meneja wa NSSF Mkoa wa Shinyanga, Shani Mtani, alisema wakijiunga wataweza kuwasaidia kuepukana na majanga yanayoikumba jamii, likiwamo la mafao ya uzeeni.

Alisema utaweza kuwasaidia wao na watoto wao, hasa katika mafao ya muda mrefu na muda mfupi.

Alisema mafao ya muda mrefu ni pensheni ya uzeeni na mafao ya muda mfupi ni kuumia kazini, uzazi na mazishi.

Alisema mafao ya muda mrefu yatamsaidia mzee kwa muda wa miaka 60 na kila mwezi anakuwa analipwa na iwapo atafikwa na mauti, familia yake itaendelea kulipwa hadi pale watoto wake watakapofikia umri wa kujitegemea na kama ana mtoto mlemavu ataendelea kupata huduma hadi mwisho wa maisha yake.

“Ndugu zangu mwanachama aweze kupata mafao haya inabidi ujiunge na uchangie shilingi 20,000 kila mwezi, hivyo msiogope mfuko huu sio wa kitapeli, unatambulika kabisa kiserikali, jiungeni ili hapo baadaye  watoto wenu waweze kufaidika na mafao hayo hata nyinyi wenyewe,” alisema Shani.

Mmoja wa wananchi, Masunga Mahenda, alisema wao hawayaamini mashirika kwa kuwa mara nyingi wamekuwa wakiogopa kutapeliwa na si rahisi walio wengi kujiunga na mfuko huo kwa kuwa kijijini hapo wanaojua kuandika na kusoma ni watu saba na kijiji hicho kina wakazi 1,500.

“Nikishajiunga na mfuko huo halafu nikapata tatizo la ugonjwa baada ya mwezi mmoja shirika litanisaidiaje na sisi huku kijijini kwetu mtu mmoja unakuta ana wanawake watatu na zaidi, je, mtu kama huyo pia shirika lita msaidiaje, tunaomba mtusaidie kwani tunaweza kujiunga kwa furaha baadaye ikawa matatizo,” alisema Mahenda.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya hiyo, Wilson Nkhambaku, aliwashauri wananchi hao kujiunga na mfuko huo kwa kuwa si wa kitapeli.

“Ninachowashauri kwa marika yote, vijana na wazee wangu tujiuge na mfuko huo utatusaidia hapo baadaye, pia katika suala la elimu tujitahidi, maana bado tuko nyuma, tusipobadilika tutakuwa tunaongozwa na watu kutoka nje kila siku, tukatae ujinga, tuwasomeshe watoto wetu tukibadilishe kijiji chetu,” alisema Nkhambaku.

Aidha, aliwashauri kuwasomesha watoto wao, hasa wa kike na kuwaeleza kuwa ng’ombe wanazowaozesha iwapo wakiwasomesha wana uwezo wa kuwanunulia kwa mwezi mmoja katika mishahara yao
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa