Home » » Mgeja asema CCM kufa ni ndoto

Mgeja asema CCM kufa ni ndoto

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga, kimekanusha kauli zinazotolewa na baadhi ya watu wakiwemo viongozi wa vyama vya upinzani, wanaodai chama hicho hivi sasa kinakaribia kufa na kwamba hizo ni ndoto za mchana. Kauli hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja alipokuwa akipokea wanachama wapya zaidi ya 200 katika kata ya Pandagichiza wilayani Shinyanga, ambao wamejiunga na chama hicho.
Mgeja alisema watu wanaodai CCM hivi sasa inachungulia kaburi na inakaribia kufa ni waongo na wapotoshaji wa ukweli kwa vile hawaoni ukweli na kwamba madai wanayoyatoa ni sawa na mtu anayeota ndoto za mchana huku akiwa anatembea.

Alisema iwapo chama hicho kingekuwa kinachungulia kaburi, hivi sasa isingekuwa rahisi kwa Watanzania makundi kwa makundi kuendelea kujiunga na kwamba idadi ya wanaojiunga na CCM inaonyesha jinsi gani ambavyo bado wanakiamini chama hicho na ni wazi wataendelea kukipa ridhaa ya kuongoza nchi.

“Hawa watu mimi hata siwaelewi nashangazwa na kauli wanaodai CCM imechungulia kaburi na inaelekea kufa, mimi nafikiri wanaota ndoto za mchana tena huku wanatembea, kama ni kufa basi ni wao watakaoanza kufa sio CCM, bado ni imara na Watanzania wengi wanaendelea kujiunga na chama chetu kila siku.”

“Ninyi wenyewe ni mashahidi, leo tumepokea wanachama zaidi ya 200, Kishapu wameingiza wanachama zaidi ya 21,000 ndani ya kipindi cha miaka mitano, lakini juzi Shinyanga mjini mwenzetu Mbunge wa mjini, Masele (Stephen) alipokea wanachama wapya 350 kutoka vyuoni, sasa huku ndiyo kufa kwa CCM?” Alihoji Mgeja.

Alisema yeye binafsi anaamini kutokana na imani waliyonayo Watanzania kwa chama hicho ni wazi kitaendelea kuongoza Serikali kwa miaka mingi kwa sababu vyama vya upinzani haviko imara na viongozi wake wanatumia muda mwingi kuwashambulia viongozi wa CCM badala ya kufanya kazi ya kuviimarisha vyama vyao.

Aidha aliwataka watendaji wa Serikali wahakikishe wanatimiza wajibu wao kwa kuwatumikia wananchi kwa kuwaondolea kero zinazowakabili katika maeneo yao, hasa upande wa sekta ya miundombinu ya barabara, maji, afya na elimu na kwamba hivi sasa kazi ya ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo uko mbioni kukamilika.

CHANZO: MTANZANIA

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa