JUMLA ya wasichana 700 wenye umri kati ya miaka 10 hadi 19
waliokatisha masomo katika shule za msingi na sekondari wilayani Kahama
kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kubeba mimba wamejitokeza
kupatiwa elimu ya Afya ya uzazi wa mpango na ujasiriamali inayotolewa
na Shirika la Kiota Women Health Development (KIWOHEDE).
Mkurugenzi wa shirika hilo, Justa Mwaituka alisema idadi hiyo ni wale
waliokatisha masomo ambao wametokea katika kata nne za Lunguya,
Shilela, Mhongolo na Busoka huku kata 55 za wilaya hiyo hali siyo ya
kuridhisha.
Alisema kuwa ili kukabiliana na tatizo hilo, shirika hilo limeanzisha
mradi wa miaka miwili ambao utawawezesha wasichana hao kurejea shuleni
ikiwemo vyuo vya ufundi na wengine elimu ya upambaji na kompyuta huku
wakianza na wanafunzi 24 watakaosoma miezi sita.
Mwaituka alisema pia shirika hilo limeanzisha utaratibu wa kuweka
kituo katika kila kata badala ya kuwapeleka wote katika sehemu moja
hatua itakayorahisisha upatikanaji wa mafunzo.
“Pamoja na mpango huo, tayari wakufunzi 38 wamepatiwa elimu ya uzazi
wa mpango kutoka vijiji 19 vya kata hizo ambao wataenda kutoa elimu
hiyo katika vijiji vyao hatua itakayosaidia kupunguza mimba za utotoni
na ukatishaji wa masomo,” alisema.
Naye muuguzi mkuu wa hospitali ya wilaya hiyo, Kalidushi Charles
alisema tatizo kubwa linalochangia wakazi wengi kuzaa bila mpango ni
kutokana na mfumo dume wa wanaume kutohudhuria mafunzo ya uzazi na
kuamini kuwa anayepaswa kuhudhuria kliniki ni mwanamke pekee.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment