Home » » UKAWA KUSUSIA BUNGE LA KATIBA:Wasomi,viongozi wa dini watoa maoni mchanganyiko

UKAWA KUSUSIA BUNGE LA KATIBA:Wasomi,viongozi wa dini watoa maoni mchanganyiko

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),Dk. Benson Bana.
 
Watu mbalimbali, wakiwamo viongozi wa dini, wasomi na asasi za kiraia, wamezungumzia wajumbe wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia Bunge Maalum la Katiba na kutoka nje, huku baadhi wakipinga hatua hiyo na wengine wakishauri Bunge hilo livunjwe.
TGNP
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) wameshauri kufanyika jitihada za haraka kunusuru  mwenendo wa Bunge hilo na hata maamuzi yatakayofanywa na wajumbe waliobaki juu ya katiba hayatakuwa ya Watanzania.

Mkurugenzi wa TGNP, Lilian Liundi, alisema hawaridhiki na mwenendo wa Bunge hilo kwa kuwa umeonyesha udhaifu mkubwa huku mambo mengi yakijitokeza hususan ubaguzi, vitisho, vijembe na unyanyasaji.

“Kwa kweli sisi haturidhiki na mwenendo mzima wa Bunge kwa sababu udhaifu mkubwa umejionyesha, kwa mfano unaposema mkichagua muundo wa serikali tatu lazima mtatawaliwa na jeshi, huko ni kuwatisha wananchi wasichague kile wanachokitaka kwa kuwafanya waogope,” alisema.

TLS YAZUNGUMZA
Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), kimesema mwenendo wa Bunge hilo unavyoendelea sasa siyo tena wa kupata Katiba ya nchi, bali ni wa kupata katiba ya chama binafsi.

Rais wa TLS, Charles Rwechungura, alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na NIPASHE juu ya mwenendo wa Bunge hilo.

Alisema kwa sasa katika Bunge hilo inatafutwa katiba itakayoisaidia chama fulani katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na kuendelea.

“Mjadala siyo tena wa kupata katiba mpya ya nchi, bali ni mjadala wa katiba ya chama kinachotaka, tunapoteza nafasi nzuri ya kupata katiba,” alisema.

AZAKI
UMOJA wa Asasi za Kiraia (Azaki) umesema iwapo hali ya kuyumbishwa na vitisho dhidi kwa wajumbe wa Bunge hilo kwa maslahi ya kisiasa halitakoma, haliwezi kutoa katiba yenye maridhiano ya wanajamii wote.

Akisoma tamko kuhusu mwenendo wa mchakato wa kutunga katiba mpya, kwa niaba ya asasi 500, Mwenyekiti wa Azaki, Irene Kiria, alisema katiba itakayopatikana ni ya watawala na siyo wananchi.

Alisema wamebaini taswira iliyopo sasa katika Bunge hilo inafifisha matamanio ya Tanzania mpya kwa kuwa haionyeshi dalili zozote nzuri za kupata katiba ya wananchi, bali ya wanasiasa.

“Malumbano yasiyo na tija na yaliyopoteza muda na rasilimali za Watanzania, kama kura za siri au za wazi wakati siku zote inafahamika kwamba, mpigakura anatakiwa kujengewa mazingira ya kuchagua kile anachokiridhia na wala siyo kwa kumridhisha mtu mwingine,” alifafanua.

THRDC
Mkurugenzi wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa, alisema kumekuwapo mazingira na kila dalili ya kutaka kulipa Bunge la Katiba madaraka makubwa yasiyostahili ya kutupilia mbali Rasimu ya wananchi na kuja na Rasimu inayopendekezwa na watawala.

Alisema kumekuwapo mazingira ya kila aina ya kuandaa wananchi kupokea katiba pendekezwa iliyotokana na rasimu isiyo ya wananchi kwa kuanza kuwajengea imani kuwa kazi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba haifai na haitekelezeki.

“Kuchafuliwa ama kudhalilishwa kwa Tume ya Katiba, ni sawa na kumdhalilisha Mtanzania aliyetoa maoni yake kwa Tume kama chombo halali cha kisheria katika mchakato wa Katiba,” alisema.

JUKATA
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Deus Kibamba (pichani), amesema baada ya baadhi ya wajumbe zaidi ya 200 kutoka jana nje ya Bunge hilo likiwa linaendelea, ilipaswa Mwenyekiti wake kusimamisha shughuli bungeni na kuitisha kamati za uongozi kujadili suala hilo.

Alisema kutokana na uzoefu wa mabunge yanayotengeneza katiba duniani, ni kuwa Bunge hilo ni la kipekee ndiyo maana wanakaa bungeni wakiwa wamejichanganya tofauti na mabunge mengine.

“Bunge hili si la kiitikadi la vyama ni bunge linalojadiliana kwa makubaliano na kufikia muafaka, maamuzi ya pamoja. Na waliotoka jana nje ya Bunge wanatajwa kuwa ni Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), si kweli waliotoka nje walikuwa na nia waliowakilisha vyama na asasi za kiraia,” alisema Kibamba.

SHEIKH ALHAD
Hata hivyo, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salumu, alisema hakuridhishwa na hatua ya wajumbe hao kutoka nje ya Bunge.

Sheikh Alhad alisema wajumbe hao hawakupaswa kususia Bunge kwani kama wana misimamo yao, wangeendelea kuvumilia bila kutoka nje kwa sababu kufanya hivyo watashindwa kuipigania.

Alisema licha ya kila mtu kuwa na uhuru wa kutoa mawazo yake, Bunge hilo linaonekana kupoteza maadili na kuonya kuwa kama wajumbe hawatabadilisha mwenendo wanaokwenda nao hivi sasa, itakuwa kazi ngumu kuwapatia Watanzania Katiba wanayoitarajia.

DK. BANA
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema fedha zinazotumika kugharimia wajumbe wa Bunge hilo ni nyingi, hivyo kitendo kilichofanywa na Ukawa si cha kiungwana.

Alisema kitendo hicho hakina tija kwa Watanzania na havipaswi kuendelea katika Bunge hilo kwa kuwa Watanzania wasingependa kuona vikiendelea.

Imeandikwa na Elizabeth Zaya, Gwamaka Alipipi, Salome Kitomari na Christina Mwakangale.
 
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa