Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Binadamu anapozaliwa hupewa jina ambalo humtambulisha au
humtofautisha na binadamu wenzingine. Hata hivyo kutokana na mabadiliko
ya sayansi, teknolojia na kijamii baadhi ya watoto hupewa majina hata
wangali tumboni mwa mama zao!
Hali hii nayo hujitokeza katika biashara, kila
mfanyabiashara angependa kuipa biashara yake jina ambalo
lingeitofautisha na biashara nyingine kwa wateja wake.
Biashara kupewa jina ni moja ya hatua ya awali ya
kurasimisha biashara husika kwani mwenye biashara atahitajika tena
kupata cheti cha biashara na namba ya mlipa kodi kutoka Mamlaka ya
Mapato Tanzania.
Hatua nyingine ni kupata leseni ya biashara kutoka
katika manispaa au halmashauri husika na kufuata taratibu nyingine
ambazo zimewekwa na mamlaka husika katika eneo lake la kufanyia
biashara.
Urasimishaji biashara ni hali ya kuifanya biashara kutambulika kisheria kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Kimsingi, jina la biashara kwa mtu binafsi
husajiriwa baada ya kuanza kufanya biashara na huwa inashauriwa kusajiri
jina la biashara angalau ndani ya siku 28 tangu kuanza kufanya
biashara, mbali na hapo mwenye biashara atahitajika kutoa sababu za
kutosajiri jina la biashara ndani ya siku hizo, ingawa pia baadhi yao
hurasimisha biashara zao kabla ya kuanza kutegemeana na utashi wa mwenye
biashara.
Katika nchi yetu na nyingine nyingi zinazoendelea,
wajasiriamali wengi wadogo na wa kati wamekuwa wakifanya shughuli zao
bila kuzirasimisha kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo kushindwa kwa
Serikali kuwa na mfumo mzuri pamoja na vivutio ambavyo vingewafanya
wajasiriamali hao kurasimisha biashara zao.
Sababu nyingine ni wajasiriamali kutoona umuhimu
wa kurasimisha biashara zao, na gharama kubwa za mchakato wa
urasimishaji biashara kama vile muda na fedha. Matokeo ya kutorasimisha
biashara kwa mjasiriamali ni kutotambulika kisheria na hivyo kuishi kama
digidigi ndani ya mbwa mwitu.
Mara nyingi kumekuwa kukijitokeza ugomvi kati ya
askari wa majiji/miji mbalimbali hapa nchini kwa madai kuwa
wajasiriamali walio wengi wanafanyia biashara zao katika maeneo yasiyo
rasmi jambo linaloashiria kuwa wajasiriamali hao wanafanya biashara
ambazo hazitambuliki kisheria.
Ugomvi huo umekuwa ukisababisha wajasiriamali hao
kupoteza mali zao walizochuma kwa shida, na imekuwa ikisababisha wengine
kupelekwa mahakamani na kuhukumiwa ama kifungo gerezani au kulipa faini
huku baadhi yao wakikata tamaa ya maisha na kurudi katika hali zao za
awali za kutokuwa na kazi.
Vilevile imekuwa ikiwawia vigumu kupata misaada
ikiwa ni pamoja na mikopo kutoka katika taasisi au watu mbalimbali
kutokana na kutokuwa na uthibitisho wa kufanya biashara kama vile mahali
maalumu wanapofanyia biashara, leseni za biashara na mambo mengine
yanayoendana na masuala ya biashara zilizo rasmi. Wajasiriamali hawa
wadogo wamekuwa hawana mchango wa moja kwa moja katika pato la taifa kwa
sababu hawalipi kodi kwa mujibu wa sheria, ikiwa ni pamoja na kuwafanya
wasikue kibiashara kwa kuogopa kulipa kodi kutokana na mazoea ya
kufanya biashara zisizo rasmi kwa muda mrefu.
Kwa kuwa dunia ya sasa imekaa kama kijiji na ili
ufanikiwa sharti hujitahidi kupambana ili ufahamike katika “kijiji hiki”
urasimishaji wa biashara kwa wajasiriamali ni muhimu sana kwani mbali
ya kuweza kupata tenda mbalimbali zinazotangazwa, na kupata habari za
biashara kutoka vyanzo vya Serikali, kunakuwa na uwezekano wa kupata
udhamini wa kuonesha na kuuza bidhaa katika maonesho tofauti.
Mwandishi wa makala haya ni mtaalamu wa Ujasiriamali na mtunzi wa vitabu
Chanzo:Mwananchi
Mwandishi wa makala haya ni mtaalamu wa Ujasiriamali na mtunzi wa vitabu
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment