Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MGODI wa madini ya dhahabu Bulyanhulu unaomilikiwa na Kampuni ya
African Barrick Gold Mine uliopo katika Kijiji cha Kakola, Kata ya
Bulyanhulu wilayani Kahama, umegawa vitabu 898 kwa shule za msingi 10
zilizo katika maeneo ya mgodi huo.
Katika hafla ya ugawaji wa vitabu hivyo uliofanyika katika Shule ya
Msingi Kakola juzi, Meneja wa mgodi huo, Peter Burger, alisema wametoa
msaada huo ili kutimiza nia yao ya kusaidia kuleta maendeleo kwa
wananchi wanaozunguka mgodi huo, hususan katika sekta ya elimu.
Burger alisema ili jamii iweze kuendelea na kukua kiuchumi, ni lazima
wananchi wake wawe na elimu ya kutosha ambayo ndiyo mwanga wa maisha
yao.
“Mgodi huu licha ya kutoa misaada mbalimbali kwa wananchi na
kuwajengea miradi ya maendeleo, hatutatenda haki endapo hatutalipa
kipaumbele suala la elimu.
“Asilimia kubwa ya wananchi wanaozungukwa na migodi hawapendi kusoma
na wamekuwa wakiomba tuwape ajira migodini bila elimu wala ujuzi wowote
hali ambayo inatuwia vigumu,” alisema meneja huyo.
Burger alizitaja shule zilizonufaika na msaada huo kuwa ni Kakola A
(vitabu 88), Kakola B (93), Kakola C (93), Bugalama (101), Busindi
(84), Ibanza (66), Iyenze (93), Buyange (97), Igwamanoni (99),
Busulwangili (84) vyote vikiwa na thamani ya sh mil. 10.
Ofisa uhusiano wa mgodi huo, Jonh Bosco, alisema Juni mwaka jana,
mgodi huo uligawa madawati 1,329 katika shule hizo yenye thamani ya sh
milioni 212.6, na kusomesha wanafunzi 900 katika shule za sekondari.
Katika shukrani zake, Kaimu Ofisa Elimu Shule za Msingi Kata ya
Bulyanhulu, Alack Mbilinyi, aliuomba uongozi wa mgodi huo kuendelea
kusomesha na kutoa msaada wa vitendea kazi vya elimu kwa wananchi bila
kuchoka.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment