Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Bunge Maalumu la Katiba linatarajiwa kuanza mnamo Agosti 5 mwaka huu, likiendeleza mjadala wa siku 70 wa rasimu ya Katiba.
Bunge hilo liliahirishwa Aprili 25 ili kupisha Bunge la Bajeti lililoisha hivi karibuni.
Kabla hata halijaahirishwa, tayari hali
ilishachafuka baada ya wajumbe wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) kutoka nje ya ukumbi wa Bunge wakilalamikia pamoja na mambo
mengine kupindishwa kwa rasimu ya Katiba.
Kikubwa wanachopigia kelele Ukawa ni kuheshimiwa kwa rasimu ya Katiba hasa suala la muundo wa Serikali ya Muungano.
Tangu Bunge hilo lilipoanza vikao vyake Februari
26 mwaka huu, mjadala umejikita kwenye muundo wa Serikali ambapo Ukawa
wanataka muundo wa Serikali tatu uliopendekezwa na rasimu ya Katiba,
huku CCM wakisisitiza serikali mbili.
Kutokana na tofauti hiyo, wajumbe wa Ukawa wameapa
kutorudi Bungeni ifikapo Agosti 5, huku kukiwa na juhudi nyingi za
kuwashawishi kurudi ikiwamo ya Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta
kuitisha vikao vya kutafuta suluhu.
Hadi sasa haijajulikana kuwa Bunge hilo litafanyikaje ikiwa wajumbe wa Ukawa zaidi ya 200 wataendelea na mgomo wao.
Lakini kwa kuwa kinachogombewa kikubwa ni muundo
wa Serikali, huku CCM wakilalamikia utendaji wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba, katika ukusanyaji wa
maoni, nadhani suluhisho ni kurudi kwa wananchi.
Turudi kwa wananchi na kuwapa fursa nyingine ya kuamua upi hasa muundo wa serikali wanaoutaka, wa serikali mbili, tatu au moja.
Tume ya Jaji Warioba ilizunguka karibu nchi nzima
ikihoji wananchi, kisha ikayachambua maoni na kutengeneza rasimu ya
kwanza na ya pili zote zikionyesha muundo wa Serikali tatu.
Sasa CCM wanaona kiama chao kimefika, wanataka kupeleka puta mchakato huo ili waendelee na Serikali zao mbili.
Pamoja na kwamba kutakuwa na kura ya maoni baada
ya Bunge hilo, nadhani suluhisho kwa sasa ni kupiga kura ya awali ya
maoni ili kuamua tu mfumo wa Serikali.
Kura hii ikishapigwa na wananchi wakiamua muundo huo, basi wajumbe warudi Bungeni waendelee kujadili vipengele vya rasimu.
Kwanza kura ya maoni kuhusu muungano, ilipaswa
kupigwa kabla hata mchakato wa Katiba haujaanzishwa. Hiyo ingeondoa
dukuduku la muda mrefu kutoka kwa wananchi kuhusu muundo wa muungano.
Muungano wenyewe una maswali mengi yasiyo na majibu hadi leo kwa kuwa haukushirikisha wananchi tangu awali.
Hii ingekuwa fursa maalumu ya kuwashirikisha
wananchi kwa kupiga kura ya maoni ya kama wanautaka muungano na uwe wa
Serikali ngapi.
Kwa hali ya sasa, hata Ukawa wakirudi Bungeni,
wataishia kutukanana na wajumbe wa CCM hadi siku 70 zitakwisha. Pesa za
walipa kodi zitaliwa bure na tusipate Katiba tunayoitaka.
Bora mchakato huo urudishwe kwa wananchi watoe suluhusho
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment