Home » » SHIBUDA AWALALAMIKIA WATAALAMU ZAO LA PAMBA

SHIBUDA AWALALAMIKIA WATAALAMU ZAO LA PAMBA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

IMEELEZWA kuwa wakulima wa zao la pamba nchini wataendelea kudorora kila mwaka kutokana na baadhi ya wataalamu wazao hilo wanaopaswa kuwasaidia wakulima hao kushindwa kutimiza wajibu wao kikamilifu.

Hali hiyo imebainishwa mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Shinyanga na mlezi wa Chama cha wakulima wa pamba nchini (TACOGA), John Shibuda katika kongamano la siku moja la wadau wa zao la pamba lililoandaliwa na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA).

Shibuda ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi Mkoani Simiyu kwa tiketi ya CHADEMA alisema wataalamu wengi wa kilimo hawajatekeleza wajibu wao kikamilifu kwa kujikita zaidi katika kuchunguza matatizo yanayowakabili wakulima wa zao la pamba ili kuweza kuyatatua.

Alisema ni wazi sekta ya pamba hapa nchini itaendelea kudorora wakati wote kutokana na watu wenye wajibu wa kuwasaidia wa kulima wa zao hilo ambao ni wasomi waliobobea kuamini kwamba wao ndiyo wanaojua zaidi na hivyo kushindwa kuwasikiliza wakulima wanaoonekana kutojua chochote.

Mbunge huyo alisema mara nyingi wataalamu hao wamekuwa wakitoa kwa viongozi wa serikali wa ngazi za juu taarifa zisizo sahihi na hivyo kujikuta wakitoa maagizo yasiyo sahihi kwa wakulima ambapo alitoa mfano wa matumizi ya mbegu za pamba zilizoondolewa manyoya (Quton) zilizogoma kuota msimu uliopita katika baadhi ya maeneo.

Sasa hali hii inayosababishwa na wataalamu walioaminiwa na serikali kwa ajili ya kuwasaidia wakulima imechangia kwa kiasi kikubwa ombwe la kutokuwepo uwazi na ukweli na hivyo kusababisha visilani vya kulaumiana kati ya wakulima na watendaji ndani ya serikali.

Msimu uliopita wataalamu wetu waliwashauri wakulima kupanda mbegu za pamba zilizoondolewa manyoya zilizosambazwa na kampuni ya Quton, palikuwa na shinikizo kubwa kutoka kwa viongozi wa serikali na hii ni baada ya kupokea taarifa za wataalamu kwamba mbegu hizo ni bora zaidi, kumbe sivyo," alisema Shibuda.

Shibuda aliwataka wataalamu watekeleze wajibu wao kikamilifu kwa kumsaidia mkulima wa zao la pamba hapa nchini ili aweze kunufaika na kilimo hicho na wawe makini wanapotoa taarifa zao mbalimbali kwa viongozi wa serikali ili kuepuka migongano inayojitokeza mara kwa mara kati yao na wakulima.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa MVIWATA mkoani Shinyanga, Charles Ndugulile alisema mtandao huo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo vijijini wanatambua changamoto zinazowakabili wakulima wa zao la pamba na hivi sasa wanafanya juhudi ya kuangalia jinsi ya kuzitatua ikiwemo suala la matumizi ya mbegu za Quton kutoota vizuri.

Chanzo:Majira

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa