Home » » TUNAPO FUNDISHA MASOMO BADALA YA MAARIFA TUTAFIKA?

TUNAPO FUNDISHA MASOMO BADALA YA MAARIFA TUTAFIKA?

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Wengi wanajiuliza, kwa nini nchi za Kiafrika bado ni maskini sana licha ya kuwa na rasilimali nyingi, wasomi wengi na hata misaada lukuki toka nchi zilizoendelea?
Nchini kwetu, enzi za awamu ya kwanza sababu ilikuwa ni kutokuwa na wasomi wengi. Hatukuwa na wataalamu wa kutosha, na hatukuwa na teknolojia muafaka; inawezekana. Je, bado hizi ni sababu hadi leo.
Tukihesabu wasomi wenye shahada lukuki waliobobea kwenye maji, ni wengi sana. Lakini, tatizo la maji liko palepale. Tena lipo hadi miji mikubwa kama Dar es Salaam. Wakati fulani Tanzania tuliagiza chakula toka nje ya nchi wakati tuna maprofesa waliobobea kwenye kilimo na ufugaji.
Uchumi unadorora kila leo wakati vyuo vikuu vinatoa maelfu ya wachumi waliobobea. Nyama tunaagiza nje ya nchi wakati wapo wataalamu wa ufugaji wengi tu. Tunaagiza hadi vijiti vya kuchokonelea meno wakati wapo maelfu ya wataalamu wa kuchonga waliozungukwa na miti mingi na mbao pomoni.
Tunaagiza China hadi sindano ya kushonea kifungo cha shati wakati maelfu ya wahandisi wa chuma wapo nchini wamejaa tele. Tunaagiza maua China wakati tunao wataalamu wa mapambo na wasokotaji. Tunapunjwa na kulaliwa kwenye mikataba ya biashara na uwekezaji wakati wanasheria waliobobea wamejaa tele. Kuna hitilafu kwenye umaizi wa wasomi wetu uliodumaza ujuzi na kukuza nadharia!
Ukihudhuria mahafali ya kutunukisha shadaha na stashahada pamoja na shahada za uzamivu katika vyuo vikuu mbalimbali, utafahamu kuwa hatuna njaa ya wasomi. Hatuna upungufu wa wataalam. Sasa iweje majibu ya matatizo yetu hayapatikani? Iweje wasomi wajae tele lakini hakuna uvumbuzi, hakuna ubunifu, hakuna ugunduzi wala hakuna ufundi unaofanywa na wasomi hao?
Kwa sasa ni kawaida kuona bibi kizee wakijijini asiyejua kusoma na kuandika anaweza kufuga kuku na ng’ombe kuzidi profesa wa ufugaji mwenye shahada lukuki? Inakuwaje wamachinga ambao hata kuandika tabu wanaweza kufanya biashara kuliko profesa wa biashara aliyebobea kwenye nadharia za biashara?
Msukuma na Mmasai aweze kufuga ng’ombe hadi elfu 2 wakati hajui kusoma na kuandika, lakini profesa wa ufugaji hawezi kufuga hata kuku mmoja? Akihitaji kitoweo anakwenda supermarket au buchani.
Inakuwaje mama wa kijijini akaweza kuchimba kisima na kuitosheleza familia maji lakini injinia aliyebobea kwenye maji hawezi hata kuvuna maji ya mvua ananunua maji supamaketi?
Inakuwaje profesa wa uhandisi wa uselemala ananunua vijiti vya kuchokonelea meno vilivyotengenezwa China na watoto wa shule ya msingi wakati yeye ana digrii nne za uselemala? Kuna tatizo kwenye elimu yetu. Elimu ya kweli ni ile inayomsaidia mtu kupata nafuu ya maisha kwa kuvumbua majibu ya matatizo na suluhu za changamoto. Kama umesoma na huna majibu ya matatizo hiyo ni elimu bandia; yaani- vyeti pasipo ujuzi wala maarifa.
Tatizo la msingi katika haya yote ni: tufundisha masomo na nadharia badala ya ujuzi na maarifa. Wakoloni hawakuleta ujuzi, hawakuletea maarifa wala ubunifu. Walituachia masomo kama vile kemia, historia, bailojia, fizikia, kilimo, ufugaji na uraia. Siyo elimu!
Tuliachiwa somo la nadharia za uchumi-pasipo ujuzi wala maairifa ya uchumi. Ndiyo maana wachumi wapo wengi lakini wameshindwa kuivusha jamii kiuchumi. Tuliachiwa somo la nadhari ya kilimo-pasipo maarifa wala uuzi wa kilimo. Ndiyo maana tunao wasomi wa kilimo ambao hawawezi hata kulima mchicha wa kutosheleza familia. Tuliletewa somo na nadharia ya historia-pasipo maarifa wala ujuzi wa historia. Ndiyo maana wengi hatujitambui tunatoka wapi, tuko wapi na tunataka kwenda wapi. Tunakimbia mbio bila kuwa na mwelekeo sahihi. Huzuni!

Tuliachiwa masomo naa nadharia za biashara. Nasi tukasomesha watoto wetu tukawaita wataalamu wa bishara-pasipo ujuzi wala maarifa ya biashara. Leo wasomi wetu wanasaini mikataba na wageni ya kuipora nchi pasipo kujua- wakilaghaiwa na wageni wenye elimu ya sekondari tu kutoka ughaibuni. Mungu atahurumie!
Kwa bahati mbaya, serikali za Afrika zimeyang’ang’ania masomo tuliyoachiwa na wakoloni tukidhani ni elimu. Kuanzia elimu ya chekechea hadi vyuo vikuu msisitizo wa elimu yetu ni masomo tuliyoachiwa na wakoloni siyo ujuzi, siyo maarifa wala uwezo wa kubuni na kufikiri. Hata vipaji asilia vya wasomi vimeuawa vyuoni kutokana na msisistizo wa masomo badala ya kujifunza.
Walimu wanahangaika kumaliza silabasi za masomo hata kama watoto hawajui kusoma na kuandika. Maprofesa vyuo vikuu wanahangaika kuwakaririsha wanafunzi nadharia hata kama wanachuo hawaelewi chochote-wanapata digrii. Tunajidanganya kwa kujisifia kuwa wasomi wengi kumbe wana elimu bandia ambayo haitusadii kusonga mbele. Masomo! masomo! masomo; yanatuangamiza Waafrika!
Walioendelea hawakuwekeza kuwafundisha watoto wao masomo na nadharia. Nchi zote walioendelea waliwekeza kwenye kufundisha watoto wao maarifa asilia katika lugha asilia na misingi ya kuibua vipawa na kuwajenga kwenye falsafa ya kuitafiti dunia. Elimu hii ndiyo imewafanya watoto wao waweza kufikiri kwa kina, waweze kuvumbua na kugundua, waweze kutafiti teknolojia na kuibua dhana mpya kila kukicha. Wamepata maendeleo

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa