Watumishi wa Serikali
wametakiwa kuzingatia sheria, taratibu na maadili ya kazi wakati wa kutimiza
majukumu yao.
Wito huo umetolewa na
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Ally Nasoro Rufunga alipokutana na waajiriwa wapya
wa Sekretarieti ya Mkoa wa Shinyanga ofisini kwake jana.
Mhe. Rufunga amesema
ili kuwahudumia wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kwa ufanisi watumishi hao
walioajiriwa hivi karibuni wanatakiwa kujifunza na kufanya kazi kwa bidii,
kuzingatia majukumu ya kazi na ushirikiano bila kuathiri sheria na taratibu za
utumishi wa umma.
Amewataka pia
kujiendeleza kielimu kwa kutumia fursa mbalimbali zilizopo ili kuinua taaluma
zao na kuongeza ufanisi katika kazi zao.
Aidha, Rufunga
amewahamasisha watumishi hao kupima Afya kila mara ikiwemo Virusi vya
UKIMWI ili wawe mfano kwa wananchi
wanaowahudumia.
Katika hatua nyingine,
Mkoa wa Shinyanga umeanza maandalizi ya kupokea na kukimbiza Mwenge wa Uhuru
mwaka huu 2014, unaotarajiwa kuwasili mkoani hapa mapema mwezi Oktoba.
Mwenge wa Uhuru mwaka
huu utapokelewa kutoka Mkoa wa Geita na utakimbizwa katika Halmashauri sita za Wilaya,
ambazo ni Ushetu, Msalala, Halmashauri ya Mji Kahama, Halmashauri ya Wilaya ya
Shinyanga, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga na kumalizia katika Halmashauri
ya Wilaya ya Kishapu ambapo utakabidhiwa mkoani Tabora kupitia Wilaya ya Nzega.
Kikao kilichofanyika jana
katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mwenge wa Uhuru unatarajiwa
kuona, kuzindua, kufungua na kuweka mawe ya msingi miradi mbalimbali kwa lengo
la kuhamasisha shughuli za maendeleo katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa
Shinyanga.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment