Home » » JK AONGOZA WAOMBOLEZAJI

JK AONGOZA WAOMBOLEZAJI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa pamoja na viongozi mbalimbali wakati wa Mazishi ya Marehemu, Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Shaaban bin Simba jana Mkoani Shinyanga
 Rais Jakaya Kikwete jana aliongoza mamia ya wakazi wa Mkoa wa Shinyanga na mikoa mingine katika mazishi ya Mufti wa Tanzania, Shekh Mkuu, Issa Bin Shaaban Simba yaliyofanyika kwenye makaburi ya Nguzonane mkoani hapa.
Mufti Simba alifariki dunia juzi katika Hospitali ya TMJ, Dar es Salaam baada ya kuugua kisukari na shinikizo la damu.
Mwili wa Sheikh Simba uliwasili jana kwenye Uwanja wa Ndege Shinyanga na kupokewa na mamia ya wananchi na uliongozwa na msafara wa magari ya polisi hadi nyumbani kwake, Majengo.
Baada ya mwili huo kuwasili nyumbani kwake saa 8.30 mchana, vilio vilisikika kutoka kwa ndugu jamaa na marafiki huku viongozi wa Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata), wakifanya kazi kubwa kuwatuliza.
Wagombea urais  wagongana
Baada mwili wa Shekh Simba kufikishwa nyumbani kwake wagombea urais kupitia CCM ambao waliwahi kuwa Mawaziri wakuu, Frederick Sumaye na Edward Lowassa walikutana na kusalimiana kwenye msiba huo na kisha wote kuketi pamoja. Lowassa ndiye aliyetangulia kufika msibani saa tisa alasiri na Sumaye aliwasili nusu saa baadaye.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambaye pia ni mmoja wa wagombea wa CCM, aliwasili kwenye mazishi hayo wakati waombolezaji wakiwa makaburini. Mazishi ya Shekh Simba yalifanyika saa 11 jioni.
Bilal aongoza  waombolezaji  Dar
Wakati shughuli za mazishi zikiendelea Shinyanga, Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal aliwaongoza viongozi mbalimbali wa Serikali, wanasiasa, mabalozi na viongozi wa dini katika ibada mahsusi kwa ajili ya msiba huo iliyofanyika kwenye Makao Makuu ya Bakwata, Kinondoni, Dar es Salaam na kuwataka Watanzania kudumisha amani, upendo na mshikamano akisema hiyo ndiyo njia sahihi ya kuendeleza mazuri yaliyofanywa na Mufti
Baadhi ya viongozi waliohudhuria ibada hiyo ni Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa, Waziri Mkuu mstaafu, Salim Ahmed Salim, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mohammed Aboud Mohammed.
Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema, Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile, Mbunge wa Ilala, Mussa Azan Zungu, mabalozi wa Sudan, Comoro, Iran na Sudan nchini na Mwenyekiti wa Kampuni ya IPP, Reginald Mengi.
Akizungumza katika ibada hiyo, Dk Bilal alisema; “Tumempoteza kiongozi muhimu ambaye alikuwa dira na alijenga maelewano mazuri sana kati ya viongozi wa dini na viongozi wa Serikali.”
Alisema Mufti Simba alikuwa mtu mwenye upendo na aliyepigania amani ya nchi na kuwataka wananchi kuhakikisha kuwa wanafuata mema ya kiongozi huyo.
“Alijitolea sana na alikuwa mlezi wa jamii na alifanya kazi yake kwa mapenzi makubwa na hakubagua mtu. Tunamuombea kwa Mungu ampumzishe mahala pema peponi,” alisema Dk Bilal.
Akizungumza kwa niaba ya wanasiasa, Profesa Lipumba alisema: “Huu ni msiba wa kitaifa kwa sababu Mufti alikuwa mtu wa watu wote, hakuwa na makuu na kubwa zaidi alikuwa na mahusiano mazuri. Tumempoteza mtu aliyewaunganisha Watanzania.”
Profesa Lipumba alisema jambo linalotakiwa kufanywa na Watanzania ni kuhakikisha kuwa wanafuata mambo mema yaliyofanywa na marehemu enzi za uhai wake, hasa upendo, amani na mshikamano.
Kwa upande wake Mengi alisema: “Mufti alikuwa rafiki wa kweli alikuwa ni kiongozi aliyemsikiliza kila mtu na alikuwa na upendo wa aina yake.”
Alisema kiongozi huyo ataendelea kuishi mioyoni mwa Watanzania kwa mema aliyoyafanya. Akitoa salamu za CCM, Zungu alisema jambo kubwa litakalomfanya amkumbuke Mufti Simba, ni jinsi alivyokuwa akiwasisitiza wabunge wa Dar es Salaam kuwajali wanyonge na maskini.
Viongozi wa dini
Katika ibada hiyo Sheikh Hemed Jalala alisema Mufti Simba hakuwa tayari kuona Watanzania wakiishi kwa matabaka na alikuwa mstari wa mbele kupinga matukio ya uvunjifu wa amani.
Akimzungizia Mufti Simba; Sheikh Yusuf Kidago alisema: “Kifo hiki kitufumbue macho na sasa tutambue kuwa hapa duniani wote tunapita na hakuna anayejua siku, saa wala tarehe. Wapo waliotawala dunia hii kwa mabavu lakini leo hawapo tena. Hapa duniani tunapendana lakini kuna siku mmoja atamuacha mwenzake. Tunachotakiwa kufanya ni kujiandaa, hapa si kwetu.”
Kauli hiyo iliungwa mkono na Sheikh Suleiman Kilemile ambaye mbali na kueleza mazuri yaliyofanywa na Mufti Simba, alisema marehemu aliwaunganisha Watanzania na atakumbukwa zaidi kwa upendo wake
Chanzo:Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa