Home » » MAENDELEO YANALETWA NA WANANCHI WENYEWE ENDAPO WATATAMBUA JINSI YA KUTUMIA LASILIMALI ZAO

MAENDELEO YANALETWA NA WANANCHI WENYEWE ENDAPO WATATAMBUA JINSI YA KUTUMIA LASILIMALI ZAO


Haihitaji kuwa na akili sana ili kuiona tofauti ya maisha kati ya miji iliyoendelea na vijijini. Hapa nazungumzia ushirikiano wa wakazi wa maeneo hayo mawili na viongozi wao wa serikali hasa kuanzia ngazi ya mtaa na kata.
Majadiliano yakiwa yanaendelea
Wakazi wengi wa mijini huwa wanabanwa na shughuli mbalimbali za kujitafutia kipato kiasi kwamba hukosa hata nafasi ya kuwafahamu viongozi wa serikali ya mtaa wao. Aina hii ya maisha hupelekea kuzaliwa kwa tabia mbaya zaidi, nayo ni kukosa muda wa kuhudhuria mikutano muhimu inavyofanyika katika mitaa yao.
Hali hii ni tofauti kwa vijijini ambapo wananchi wengi mwenendo wa maisha yao ya kila siku kutoka kwa viongozi wao kuanzia ngazi ya kijiji, kitongoji na kata. Kutokana na aina hii ya maisha inawafanya wawe na umoja, kuishi kwa ushirikiano na kufanya maamuzi kwa pamoja hasa juu ya rasilimali zao.
Katika miaka ya hivi karibuni wanakijiji wengi wanaoishi katika maeneo yenye rasilimali wametambua umuhimu wa kutunza na kutumia rasilimali zao vizuri kwa maendeleo yao na kwa manufaa ya vizazi vijavyo. Lakini si kila sehemu hali ipo hivyo katika baadhi ya maeneo wanakijiji wamekuwa hawazitambui haki zao za msingi kutokana na uelewa mdogo.
Mwalimu kaziro Nyangisa akisoma moja ya mikataba
Mwime ni kijiji kilichopo katika kata ya Mwendakulima wilayani Kahama, mkoani Shinyanga. Wakazi wengi wa kijiji hiki ni wakulima wadogo wadogo, wafugaji na ni wachimbaji wa madini. 
Kijiji hiki ndicho kilichohifadhi mgodi maarufu wa dhahabu wa Buzwagi, uliochangia kwa kiasi kikubwa kupanda kwa hadhi ya kijiji hicho na kuwa mtaa. Hivyo kwa sasa Mwime ipo kwenye halmashauri ya mji kutokana na upatikanaji wa huduma muhimu karibia zote kuanzia huduma za afya, barabara, umeme na maji safi.
Awali kijiji cha Mwime kilikuwa kikimiliki leseni mbili za machimbo ya uchimbaji dhahabu ya Majimaji na Zanzibar. Wachimbaji wadogo wadogo walikuwa ndio walengwa wakubwa, ambapo walilipa ushuru kwa serikali ya kijiji. Na wao kunufaika na shughuli hizo ambazo zilikuwa zinawaingizia kipato.  
Uraghbishi umesaidia kupata Barabara nzuri
Ilipofika mwaka 2007 kampuni ya Pangea ilipata leseni ya kufanya utafiti na mwisho wa siku kuingia mkataba na serikali ya kijiji cha Mwime. Katika kipindi ambacho uwekezaji ulikuwa unafanywa katika eneo hilo ambalo sasa ni mgodi wa Buzwagi, kijiji kililipwa kiasi cha shilingi za kitanzania 12,000,000 kwa mwaka ikiwa kama malipo ya kusitisha uchimbaji katika eneo hilo.
Uraghbishi umesaidia kuleta umeme katika mtaa wa Mwime
Miaka miwili baadaye yaani mwaka 2009, ndipo kijiji kilipokabidhi rasmi leseni zake kwa kamishina wa madini na kuingia mkataba na Pangea (Barrick). Kwa mujibu wa kifungu namba 1.1 cha Makubaliano ya Nyongeza ya Mkataba baina ya Kampuni ya Madini ya Pangea (Barrick) na Kijiji cha Mwime; kampuni itakuwa ikikilipa kijiji kiasi cha Tsh milioni 60/- kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano na kisha pande mbili hizi zitakaa pamoja na kupitia kiwango hiki kwa kadri ya uzalishaji utakavyokuwa kwa nia ya kuboresha zaidi.
Hizi ni Nyumba mbili zilizojengwa kwa ajili ya walimu
Malipo haya yalitakiwa kuanza kulipwa kuanzia mwaka 2009 miaka miwili baada ya makubaliano kusainiwa tarehe 21 mwezi Aprili mwaka 2007. Ni mwaka 2012 malipo haya yamelipwa kwenye akaunti ya kijiji, kiasi hicho cha shilingi milioni 300/- ni malipo ya miaka mitano ya awamu ya kwanza; mkataba unatamka kila baada ya miaka 5 pande mbili (Kijiji na Mgodi) zitakaa kupitia kiwango hiki ili kuboresha kiwango hiki kutegemeana na uzalishaji.

Malipo haya yanafanyika, baada ya juhudi kubwa kufanywa na wananchi wa kijiji cha Mwime na viongozi wao katika kufuatilia fedha hizo. Na tatizo halikuwa upande wa mgodi wa Buzwagi, bali ni wananchi wa kijiji cha Mwime wenyewe kushindwa kuhimiza uongozi wao kuchukua hatua za kufuatilia suala hilo. Na hivyo kupita miaka miwili bila kitu chochote kufanyika kuanzia 2009 hadi 2011.
Hizi ni nyumba mbili  ambazo zimejengwa kwa ajili ya wauguzi

Kwa mujibu wa kifungu cha 1.2 cha Nyongeza ya Mkataba wa Makubaliano, fedha zitakuwa zinalipwa kupitia Bodi ya Wadhamini, ambayo inaundwa na wawakilishi wa kijiji, mgodi na serikali ngazi ya wilaya kama msimamizi.

“Lilitolewa tangazo kwa ajili ya watu kuomba nafasi ya kuwa wawakilishi wa kijiji kwenye Bodi, ila waliotakiwa ni wale walio chini ya miaka 60 na waliomaliza kidato cha nne. Nilipata hisia kwamba tangazo limebagua baadhi yetu wenye uwezo ila hatuna sifa walizozitaja,” anaelezea Maimuna Said mmoja wa waraghabishi wa kijiji hiko.

Wanakijiji wa Mwime pia wanafanya shughuli za kilimo na ufugaji
Hivyo wakati wa mkutano wa kijiji mwaka 2011 wanakijiji walitaka maelezo ya ziada kuhusu uundwaji wa Bodi ya Wadhamini pamoja na majukumu yake. Ndipo ilipojulikana kwamba tayari kuna watu wameshaomba nafasi hiyo na tayari wameshachanguliwa na zaidi Bodi hiyo ina mamlaka ya mwisho ya kuamua matumizi ya fedha itakazolipwa kijiji.
Uraghbishi huo ulipelekea kamati iliyokuwepo kuvunjwa na wanakijiji walioamua kuchagua viongozi wao wanaowataka na kupelekea kupata malipo yao vizuri na kufanyia maendeleo ya kijiji. Jitihada hizo zilimvutia aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Lembeli kuchangia fedha kwa ajili ya kufungua akaunti ya kijiji ya maendeleo.
Sehemu ya fedha hizo (milioni 300/-) zilitumika katika kufungua miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na Tsh 78,000,000 kutumika kujenga nyumba mbili za kuishi wauguzi, kuvuta umeme kijijini hapo na kujenga barabara huku Tsh 7,000,000 zikitumika kulipa fidia kwa watu waliokuwa na miti na makaburi sehemu ambayo barabara hiyo ilipita.
Mbali na hayo Tsh 1,800,000 zilitumika kuwalipa posho wafanyakazi wote walioshiriki kufanya kazi hiyo, yote hayo yaliweza kufanikiwa kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na walaghabishi.
Mgodi umesaidia hata wanakijiji kuwa na vitega uchumi vyao wenyewe
Waraghbishi mwalimu Kaziro Nyaingisa na mkulima Maimuna Said, wakirishirikiana na wanakijiji cha Mwime kupitia kamati iliyochaguliwa kupigania mkataba mpya na kampuni ya Accacia iliyowekeza kwenye mgodi huo baada ya Barrick. Katika mkataba mpya wa mwaka 2015/2016 umeongezeka kwa asilimia 50% kutoka Tsh 60,000,000 kwa mwaka mpaka kufikia Tsh 90,000,000 ambapo mpaka sasa fedha hizo zimeshaingia kwenye kamati na zinaendelea kutatua matatizo ya kijiji.
Kama hiyo haitoshi, Uraghbishi huo umewafanya wawekezaji wa mgodi wa Accacia kutoa ajira za utunzaji wa mazingira kwa wanawake ambao wanaishi jirani na mgodi, huku wakitengeneza matundu ya vyoo vya kisasa 16 kwa ajili ya wanafunzi wa shule ya msingi Mwime. Wameahidi pia kuongeza idadi ya visima vya pete na nyumba za walimu.
Kutokana na waraghbishi kupaza sauti zao imewasaidia wanakijiji hasa raia wa kawaida kuwa na uwezo mkubwa wa kujitambua, kujua haki zao na uhalisia katika jamii. Wametambua nini maana ya uzalendo, umuhimu wa ushirikiano, watu kuishi kwa amani, na kufanya kazi bila woga.
Kupitia uraghbishi wanawake wamekuwa sio waoga tena katika kijiji cha Mwime, hiyo imesababisha mpaka vijiji vingine kama Kilago na Nyandekwa. 

Imeandaliwa na Fredy Njeje wa Blogs za Mikoa

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa