WATUMISHI wawili wa kituo cha afya Lyabukande katika Halmashauri ya
wilaya ya Shinyanga wamesimamishwa kazi kwa uzembe uliojitokeza baada ya
mjamzito kujifungulia kwenye varanda hivi karibuni.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake hivi karibuni,
aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ambaye amehamishiwa jijini
Mwanza, Kiomoni Kibamba alisema baada ya kupata taarifa hizo waliunda
tume ya kwenda kuchunguza na kubaini uzembe ndiyo ulisababisha mjamzito
kujifungua kwenye varanda.
Kibamba alisema hivi sasa wamewasimamisha kazi na kuwafungulia
mashitaka ya kimaadili ya utumishi na kuwapa siku 14 kwa utaratibu wa
ajira ya utumishi.
Aliwataja watumishi hao ambao ni Muuguzi Msaidizi, Zufa Musa na Peter
Mazengo wa kitengo cha maabara kuwa ndio walikuwa zamu siku hiyo na
kwamba walishindwa kumsaidia mzazi kitendo kilichobainika ni cha
makusudi na uzembe.
“Nilikwisha tamka siku nyingi awamu hii ya tano ni awamu nyepesi kwa
kufanya kazi sababu imenyooka na iko wazi na mtu akienda kinyume
anatakiwa kupisha ili wabaki wanaotekeleza majukumu yao kwa mujibu wa
sheria, kanuni na katiba ya nchi kwa kuwatumikia wananchi,” alisema
Kibamba.
Hata hivyo, kamati iliyoteuliwa ikiongozwa na mganga mkuu wa wilaya,
Dk Athuman Pembe ilieleza kuwa baada ya mzazi kujifungua, watumishi hao
walipata taarifa na kwenda kumhudumia yeye na mtoto akiwa na afya nzuri
mwenye uzito wa kilo tatu na baada ya muda aliruhusiwa kurudi nyumbani.
Diwani wa Kata ya Lyabukande, Joseph Misiri, alisema aliyejifungulia
nje katika varanda la kituo hicho ni Magreth Charles (22) aliyefika
kituoni hapo akiwa ameongozana na mama mkwe.
Inadaiwa baada ya kufika kituoni hapo saa 7:00 mchana, walielezwa
hakuna huduma na siku hiyo walishauriwa waende hospitali zingine kabla
ya saa 9.30 alasiri kujifungua.
Mtendaji wa kata ya Lyabukande, Julius Lugende alisema kuwa kituo
hicho kimekuwa kikilalamikiwa na wananchi kwa kile kinachodaiwa baadhi
ya watumishi wake hawahudumii vizuri.
Chanzo Na Habari Leo
0 comments:
Post a Comment