Home » » ‘MATEJA’ WAGEUKIA UJASIRIAMALI

‘MATEJA’ WAGEUKIA UJASIRIAMALI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
WATUMIAJI wa dawa za kulevya wanaopelekwa kwenye Hospitali ya afya ya akili na utengamao ya Lutindi iliyopo wilayani Korogwe mkoani Tanga, wamegeuka kuwa mafundi baada ya kufundishwa namna ya kutengeneza samani na kapeti.Vitu ambavyo wamekuwa wakivitengeneza ni viti vyamajumbani, hotelini, kapeti za chini ya miguu na vitu ambavyo
vinatumiwa na wananchi katika matumizi yao, jambo ambalo linawafanya kujiandaa na kujiajiri wakati wanapomaliza matibabu yao.
Akizungumza jana, Muuguzi Msaidizi wa Hospitali hiyo, Amina Ramadhani, alisema baada ya kuwapokea wagonjwa hao wanakaa nao kwa kipindi fulani na watakapokuwa wamepata nafuu watawafundisha namna ya kujifunza ufundi wa kutengeneza samani.
Alisema miongoni mwa vitu ambavyo wamekuwa wakifundishwa ni kutengeneza bidhaa hizo ambazo soko lao kubwa lipo kwenye wilaya za Bagamoyo, ikiwamo maeneo mengine ndani ya Tanzania.
“Unajua tunapowapokea wagonjwa hawa sisi kama hospitali baada ya kuona wamepata nafuu kidogo, tunaamua kuwaingiza kwenye suala la ufundi seremala ambapo asilimia kubwa wamekuwa wakifanya vizuri badala ya kukaa bila kufanya kazi,” alisema.
“Lakini tunaweza kusema hili ni moja kati ya mafanikio yetu makubwa kwani mgonjwa anapokuja kwenye hospitali hii mara nyingi unakuta anashinda wodini tu, lakini anapopata nafuu basi wanaingia kwenye mambo ya ufundi,” alisema.
Alisema sababu kubwa ya kuingia kwenye shughuli za ufundi wanapokuwa huko ni kuwaandaa wakati wanapopona na kwenda kwenye jamii waweze kujiajiri kutokana na ujuzi ambao wanakuwa wameupata.
Alisema wagonjwa hao wanapokuwa wakifundiswha masuala ya ufundi inawasaidia kuondokana na utegemezi mara baada ya kupona ambao hurudishwa walipotoka.
Akizungumza mmoja wa wagonjwa wanaohudumiwa na hospitali hiyo, Abdi Mohamed ambaye alitoka Wilaya ya Kigamboni, Dar es Salaam alisema suala la kufundishwa ufundi wa kutengeneza vitu mbalimbali limewapa mwanga wa kijiajiri.
“Kwa kweli hii ni fursa nzuri kwetu kwani si kwamba inatujenga bali pia kutuandaa kuona namna bora ya kujiajiri wakati tunapotoka hapa baada ya kupona.
“Lakini pia niwaase vijana wenzangu kuachana na matumizi ya dawa za kulevya kwa sababu si mzuri na yameharibu maisha ya watu wengi kwenye jamii wanazotoka,” alisema.

Chanzo:Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa