MAJAMBAZI watano waliohusika katika mauaji katika maeneo ya Kibiti na
Mkuranga mkoaniPwani, wameuawa kwa kupigwa risasi na Jeshi la Polisi
wilayani Kahama mkoani Shinyanga walipokuwa wakitaka kufanya jaribio la
kuwapora wafanyabiashara wa dhahabu wakijibizana risasi na Polisi.
Watu hao wameuawa juzi eneo la Mwanva, Kata ya Nyahanga mjini hapa
baada ya majibishano ya risasi baina yao na askari Polisi wa doria
waliokuwa zamu katika eneo hilo. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga,
Simon Haule alisema hayo katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa
Kahama, Shinyanga ambako miili yao imehifadhiwa kusubiri kutambuliwa na
ndugu zao.
Kamanda Haule alisema mauaji hayo yametokea saa 3.00 usiku baada ya
jeshi hilo Kitengo cha Intelejensia kupata taarifa ya kuwa kuna
majambazi ambao walikuwa wamejipanga kuvamia wafanyabiashara wenye
maduka pamoja na wale wanaojihusisha na ununuzi wa madini ya dhahabu.
Alieleza baada ya Polisi kupata taarifa hizo, askari walienda katika
eneo hilo ambalo lilikuwa na vichaka pamoja na mapango ambayo
yalisababishwa na uchimbaji holela wa mchanga na walipofika walianza
kurushiana risasi kabla ya kuwazidi na kuwakamata majambazi hao wakiwa
wamejeruhiwa vibaya. Alisema majambazi hao walijeruhiwa vibaya na wakati
wakipelekwa Hospitali ya Halmashauri ya Mji, wote watano walipoteza
maisha.
Alisema baada ya kuuawa na kupekuliwa, walikutwa na bunduki moja aina
ya Short Machine Gun (SMG) yenye risasi 25 pamoja na mabomu mawili ya
kurushwa kwa mkono. Aliwaomba wananchi kuhakikisha wanashirikiana na
Polisi kutoa taarifa nzuri kama hizo ili kuwabaini wahalifu waliopo
katika jamii inayowazunguka na kuongeza suala la uhalifu ni la mtandao
mkubwa.
Alisema jeshi hilo kwa sasa limejipanga kikamilifu katika kukabiliana
na masuala ya uhalifu na kuongeza kuwa kama kuna watu wanahusika na
uhalifu ni bora wakajisalimisha pamoja na zana walizonazo. Aliwataka
ndugu wote ambao wanahisi hawajaonana na watu wao wa karibu kujitokeza
kutambua miili ya watu hao kwani mpaka sasa hawajulikani ni wenyeji wa
wapi nchini, hali ambayo inaweza kufanya miili kukaa muda mrefu katika
eneo hilo la kuhifadhia maiti.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment