Home » » MADIWANI WA KISHAPU WAMLALAMIKIA MBUNGE

MADIWANI WA KISHAPU WAMLALAMIKIA MBUNGE


Na Editha Edward, Shinyanga
MBUNGE wa Kishapu wilayani Shinyanga, mkoani Shinyanga, Seleman Nchambi amelalamikiwa na madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo kwamba aliwadhalilisha wananchi akidai kuwa ni wezi.

Hayo yalielezwa jana katika kikao cha Baraza la Madiwani, kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo, ambako walisema wamechoshwa na malalamiko hayo, hivyo wameamua kusema hadharani ili wananchi wasikie.

Madiwani pia wanamtuhumu Mbunge huyo kuwa amekuwa akitoa ahadi hewa ambazo mpaka sasa hajazitekeleza, likiwemo suala la kusomesha watoto 500 kutoka jimboni humo, lakini mpaka sasa hakuna ahadi yoyote aliyoweza kuitimiza.

“Tunashindwa kumwelewa Mbunge huyu mpaka sasa kwa sababu ubunge wake ndio unayoyoma, ina maana atawasomesha lini hawa wanafunzi aliowaahidi, maana tumesubiri hatuoni chochote, ina maana alidanganya wananchi wake?” alihoji Diwani wa Kata ya Luhumbo, Paul Magembe.

“Haya yaliyosemwa tuna ushahidi nayo na tulikuwepo wakati anayasema, hivyo tunashindwa kufanya kazi kwa sababu Mbunge wetu anaturudisha nyuma, tukipanga hivi anakuja anapangua pamoja na kutudhalilisha kuwa sisi ni wezi,” alisema Magembe.

“Tunaomba aandikiwe barua na aonywe asirudie tena kupinga maamuzi yetu, siyo siri, hata Kaimu Mkurugenzi, Eng Lukas Said alikuwepo, wala si uongo, tunaomba sasa kwa vile ni diwani mwenzetu tuchukue hatua, anatudhalilisha,” alisema Daud Matungwa, Diwani wa Kishapu.

Diwani wa Kata ya Shagihilu, alisema wakati huu ni wa kusema ukweli, kwa sababu serikali inatoa fedha kupitia Mfuko wa Mbunge, lakini amekuwa akiambatana na katibu wake bila kuchukua wataalamu wowote, hivyo akifika huko anawadanganya wananchi kuwa ametoa yeye, bila kusema ni serikali.

Diwani wa Kata ya Lagana, Boniface Butondo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, alikiri kusikia malalamiko juu ya mbunge huyo.

“Matatizo kuhusu mbunge wetu ni mengi, tumeyasikia na yamekuwa hayatujengi, naomba kwa wakati huu hatuwezi kuchukua maamuzi yoyote, ila viongozi wa maadili tutakaa na ni wajibu wake akiitwa aje, asipokuja madiwani watachukua wajibu wake,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Justin Sheka, aliwaomba madiwani wapunguze jazba ili kamati ya maadili ije ifanye kazi yake.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa