Home » » SACCOS YAIDAI HALMASHAURI YA SHINYANGA MILIONI 48/-

SACCOS YAIDAI HALMASHAURI YA SHINYANGA MILIONI 48/-

Na Editha Edward, Shinyanga
HALMASHAURI ya Wilaya ya Shinyanga inadaiwa jumla ya Sh milioni 48 na Chama cha Mikopo na Akiba (SACCOS) cha watumishi wa halmashauri hiyo zilizotoka Hazina na kufikia mikononi mwa halmashauri na kuzitumia bila makubaliano yoyote.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu wa SACCOS hiyo, Audifasi Matina, katika mkutano mkuu uliofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo na kuelezwa kuwa imepata hasara ya Sh milioni 13 kutokana na kukosekana kwa fedha za kukopeshwa kwa wakati.

Alisema Sh milioni 48 zilizotoka Hazina ambazo ni makato yatokanayo na fedha zao zilizofika halmashauri na uongozi ulizitumia bila ya kutoa taarifa katika uongozi wa SACCOS hiyo hadi walipokwenda Hazina na kupatiwa taarifa kuwa zilirejeshwa katika halmashauri.

“Fedha hizo ziko kwa mkurugenzi hivyo kinachotakiwa tupatiwe ufafanuzi na tuelezwe ni lini tutarejeshewa kwa kuwa hali hiyo imefanya Saccos kushindwa kutoa mikopo kwa wakati na kupoteza jumla ya shilingi milioni 13,” alisema Matina.

Alisema kutokana na changamoto hiyo, wamejitahidi kupiga hatua kwa kujiwekea mkopo wa dharura kwa wanachama wake ingawa bado inakabiliwa na madeni mengi yaliyosababishwa na wanachama wake kukopa fedha nyingi na kutorudisha kwa wakati.

Kwa pande wao, wajumbe Martius Balele na Honorius Lyaruu, walisema kitendo cha fedha hizo kupitia katika akaunti ya halmashauri bila idhini ya wanachama huo ni wizi hivyo ni lazima zirejeshwe na hatimaye waweze kukopa.

Naye, Mweka Hazina wa Halmashauri hiyo, Saidi Lihiyuka, alikiri kuwapo kwa deni hilo na kuahidi ndani ya miezi mitatu litakuwa tayari limerejeshwa hivyo wanachama wasiwe na wasiwasi na kama ikifika muda huo halijarejeshwa wachukue hatua ya kwenda mahakamani.

“Halmashauri ina madeni mengi ila mkurugenzi hajakaidi kulipa kama mnavyodai hivyo nchi nzima halmashauri bado hazijapewa fedha kutoka Serikali kuu, zinajitegemea zenyewe kwa vyanzo vya mapato ya ndani hadi sasa hatujapata fedha ila tunategemea ndani ya miezi miwili kupata,” alisema Lihiyuka.

Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa