Home » » SERIKALI YASHAURIWA KUREKEBISHA SHERIA YA MADINI

SERIKALI YASHAURIWA KUREKEBISHA SHERIA YA MADINI

Na Sam Bahari, Shinyanga
SERIKALI imeshauriwa kuitazama upya sheria ya madini ya mwaka 2010 na kuifanyia marekebisho na hatimaye iweze kuwanufaisha wananchi wanaolipwa fidia ya kupisha uchimbaji wa madini katika maeneo wanayoyamiliki.

Ushauri huo ulitolewa mjini hapa hivi karibuni na Mbunge wa Kishapu, Suleiman Nchambi (CCM).

Alisema sheria ya madini ya mwaka 2010 inazuia kumlipa mwananchi mali iliyo chini ya ardhi anayoimiliki, ukiwamo udongo wenye kokoto, mawe na madini mbalimbali na badala yake sheria hiyo inaelekeza kuwalipa wananchi fidia ya nyumba na miti iliyopo juu ya ardhi katika maeneo wanayoyamiliki.

Alisema licha ya sheria hiyo kuzuia kulipwa wananchi fidia ya mali zilizo chini ya ardhi, lakini pia imekaa kimya bila ya kuwaelekeza wawekezaji waanze kufunga mikataba na kuingia ubia na wananchi katika migodi hiyo kwa lengo la kuendelea kulipwa.

“Ndugu zangu mkizisoma sheria za madini mtashangaa maana zinasikitisha, kwa sababu haziwanufaishi wananchi wazawa, bali zinawakumbatia wageni wanaokuja nchini kuwekeza katika sekta ya madini.

“Huwezi kuamini kuwa kuna baadhi ya migodi ilianzishwa katika wilaya au mkoa fulani, lakini uchimbaji wake chini ya ardhi ulikwisha sambaa hadi wilaya au mkoa jirani,” alisema Nchambi.

Aliishauri Serikali kuwapatia leseni baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini aina ya gypsum, ambayo ni malighafi inayotumika kutengenezea saruji na kuwanyang’anya leseni wachimbaji hao ambao walichukua maeneo makubwa na kuendelea kuyakumbatia kwa muda mrefu bila ya kuchimba madini hayo.

Alisema kama Serikali itayarejesha maeneo hayo na kuyatoa kwa wachimbaji wadogo, viwanda vya saruji vitaongezeka, ajira zitaongezeka na hatimaye kuongeza pato la mtu mmoja mmoja.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa