Home » » WALEMAVU WATAKA WABUNGE KATIBA MPYA

WALEMAVU WATAKA WABUNGE KATIBA MPYA


na Ali Lityawi, Kahama
WATU wenye ulemavu wametaka katiba mpya kuwa na kipengele kitakachowapa fursa ya kuchagua wawakilishi kutoka katika makundi yao ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano, ambao watasaidia kujali maslahi yao.
Pendekezo hilo lilitolewa na Mratibu wa watu wasioona mkoani Shinyanga, Michael Nkanjiwa katika semina ya siku mbili juu ya ushiriki wa watu wasioona katika mchakato wa kupata katiba mpya, iliyofanyika Kata ya Mhongoro wilayani Kahama na kuwashirikisha wajumbe kutoka wilaya za Kishapu, Shinyanga Vijijini na Kahama.
Nkanjiwa alisema, mahitaji ya kila Mtanzania kwa sasa, hususani watu wenye ulemavu nchini, ni kuiona Tanzania inajengwa na kila kada bila baadhi ya makundi kuwa tegemezi.
“Hii sheria namba mbili ya mwaka 1982, inayodai walemavu tunahitaji matunzo na misaada imepitwa na wakati, wanaohitaji matunzo na msaada ni wazee na vikongwe, sio sisi vijana japo ni walemavu. Tunastahili kujengewa uwezo, ili tuweze kuchangia pato la Taifa,” alisema Nkanjiwa.
Alisisitiza, walemavu hawahitaji huruma kutoka katika vyama ambavyo uwakilishi wao huzingatia matakwa ya mwajiiri wao wa kutetea sera za chama badala ya kutetea kundi la walemavu, hivyo wanahitaji kipengele katika katiba kitachotambua uwakilishi wao kuanzia ngazi za chini hadi bungeni na kuwepo na waziri kutoka miongoni mwao.
Naye Mwenyekiti wa watu wasioona Wilaya ya Kahama, Boniventure Anthony, alisema huu ni wakati muafaka kwao kujitokeza kutoa maoni yao na kwamba serikali haipaswi kuyapuuza kutokana na kuwa dira kwao ya kujikwamua kutoka katika maisha ya utegemezi.
Mwezeshaji katika semina hiyo iliyofadhiliwa na The Foundation Civil Society, Mwalimu Jane Mugusi, aliwakumbusha walemavu kuwa wanastahili kupata stahiki mbalimbali kwa kupewa kipaumbele kulingana na ulemavu wao, ikiwemo masuala ya kuchagua na kuchaguliwa sambamba na elimu na ajira.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa