Home » » SHIRECU KUTUMIA MFUMO WA STAKABADHI GHALANI

SHIRECU KUTUMIA MFUMO WA STAKABADHI GHALANI

Suzy Butondo, Shinyanga
HATIMAYE Chama  Kikuu cha Ushirika mkoa wa Shinyanga(Shirecu1984 Ltd), kitaanza kutumia  mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani (WHRS).Mfumo huo utafanyika kupitia kwa  baadhi ya vyama vyake vya msingi vya biashara ya mazao  (AMCOS) kuanzia msimu wa 2012/3.
 Maamuzi hayo yalifikiwa  juzi na wajumbe 335 kutoka AMCOS, 455 wanachama walio hai wakati wakishiriki mkutano mkuu wa 21 wa chama hicho mjini Shinyanga.
 Akizungumza na gazeti hili,  Meneja Mkuu wa chama hicho, Joseph Mihangwa  alisema  wajumbe walifikia uamuzi huo wakati wakichangia hoja ya bei ya zao la pamba inayobadilika mara kwa mara kupelekea  wakulima kuuza kwa bei ya hasara wakati bei yazao hilo inaposhuka katika soko la dunia.
 Mihangwa alisema, wakulima wa vyama vitakavyoteuliwa kuanzia msimu wa 2012/13 watatunza pamba yao katika maghala ya watunza ghala baada ya kupima uzito halisi wa pamba hiyo na kuwalipa wakulima wanachama wa AMCOS sehemu ya fedha za mauzo.
 Hatua itakayofuata ni mkulima aliyehifadhi pamba ghalani atauza pamba yake bei ya soko la dunia itakapokuwa imeboreka, na kulipwa malipo ya pili yaani fedha zake zote zilizobakia kwa mujibu wa bei ya soko la dunia.

Wakionyesha mashaka juu ya SHIRECU kuingia tena kwenye mfumo huu ambao hapo nyuma ulisababisha baadhi ya wakulima binafsi na AMCOS zao kupoteza mamilioni ya fedha baada ya kuuza pamba yao kwa mfumo huu, mmoja wa wajumbe hao Amos Kulwa kutoka wilaya ya Maswa alisema miaka ya 2008/09 baada ya serikali ya mkoa chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa Brigedia Jenerali Yohana Balele kwa baadhi ya AMCOS zilizoteuliwa kufuata mfumo huu yasije kutokea tena.

 Alisema kuwa matokeo mabaya yaliyojitokeza katika kipindi hicho cha majaribio ya mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani ni pamoja na wakulima wa AMCOS ya Seng’wa wilayani Maswa kupoteza Sh42 milioni zikiwamo (Sh39milioni ) za malipo ya pili kwa wakulima na nyingine Sh2.3milioni  za ushuru wa AMCOS kushindwa kulipwa baada ya Mwendesha Ghala aliyeteuliwa na serikali ‘Sibuka FM’ kutokomea nazo.
 Mkutano huo mkuu uliambatana na uchaguzi wa  mwenyekiti na wajumbe ambapo Robert Jongela, aliyemaliza kipindi chake alirejeshwa kwa kupata a (361) za ndiyo,  hapana (5) na (8) zikiharibika, Thomas Masunga, kutoka wilaya ya Kahama akapewa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Union,huku  Boniface Butondo  Kishapu akishinda nafasi ya ujumbe.
Chanzo: Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa