na Ali Lityawi
KLABU ya waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga (SPC), imeungana na klabu za mikoa mingine nchini kususia kuandika habari zinazohusu Jeshi la Polisi nchini, huku ikimtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi, ajiuzulu kufuataia vitendo vya mauaji vinavyofanywa na askari wake.Katika tamko lao lililotolewa na Makamu Mwenyekiti, Isaac Mbwaga, SPC wameeleza kusikitishwa kwao na vitendo vya mauaji ambavyo vimekuwa vikifanywa na askari katika matukio mbalimbali ya mikusanyiko halali ya watu ikiwemo ya kisiasa, hususan ya hivi karibuni ya mkoani Morogoro na Iringa.
Aidha, klabu hiyo imemuomba Rais Jakaya Kikwete kuwawajibisha Mkuu wa Jeshi hilo, IGP Said Mwema na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, kutokana mauaji ya mwandishi wa kituo cha runinga cha Channel Ten, Daudi Mwangosi.
Mbwaga aliongeza kuwa SPC inaunga mkono msimamo wa Klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Iringa, kususia kuandika habari zinazohusu Jeshi la Polisi nchini mpaka pale serikali itakapowawajibisha viongozi hao waliotajwa kufuatia kifo cha Mwangosi.
“SPC tunakilaani vikali kitendo hicho cha kinyama kilichotekelezwa na askari kinyume cha sheria na wajibu wao wa kumlinda raia na mali zake. Kwa umoja wetu tunatambua mchango mkubwa wa waandishi wa habari katika kuhabarisha na kuelimisha umma, hivyo tunamtaka Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa kuwajibishwa mara moja na serikali kuhusiana na tukio hilo,” alisema.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment