Home » » WAKULIMA WA PAMBA WALALAMIKIA MIZANI YA DIGITALI

WAKULIMA WA PAMBA WALALAMIKIA MIZANI YA DIGITALI



Na Editha Edward, Shinyanga
WAKULIMA wa Vijiji vya Mwalukwa, Nzululu, Lyabusalu, Zoza na Zonza, Iselamagazi na Pandagi Chiza mkoani Shinyanga, wamelalamikia mizani ya digitali na kueleza inawapunja kutokana na kutopatiwa mafunzo ya namna inavyofanya kazi.

Wakulima hao wanaolima pamba walisema hawaitaki mizani hiyo na wanaitaka ya rula ambayo wameizoea.

“Sisi tunaona kama hawa wanunuzi wanatuibia kwa kuwa mizani gani anaona mnunuzi bila ya kuona muuzaji, halafu kwetu ni kitu kigeni, wangetuonyesha kwanza namna ya upimaji ndipo tukubaliane nao, lakini sasa tunaona wanatuibia,” walisema wakulima hao.

Shija Masalu, anayeishi Kijiji cha Mwalukwa, alisema hawajapatiwa mafunzo kuhusu mizani hiyo na wanaomba kurudisha mizani ya rula waliyoizoea.

Naye, Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Shinyanga (SHIRECU), Joseph Mihangwa, alisema wakulima wanaitaka zaidi mizani ya rula kwa kuwa wakati wanapima wanaona wenyewe, lakini ya digitali upimaji wake ni mgumu.

“Hiyo mizani ya digitali inatumia nguvu ya umeme, isitoshe wakulima hawana uzoefu nayo, kilichokuwa kinakimbiwa katika mizani ya rula ni nyepesi kuchakachuliwa kuliko hii, ijapokuwa kuna tetesi kuwa nayo imeanza kuchakachuliwa,” alisema Mihangwa.

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Shinyanga, Luppy Shirima, alisema mizani inayotumika ni mizani ya rula, lakini Serikali iliona badala yake kutumia mizani hiyo ambayo ni nyepesi kuchakachuliwa na rahisi kuenea kila mahali.

Alisema baadhi ya kampuni zilikubali kununua mizani hiyo, ingawa wamenunua kiasi kidogo ukilinganisha na wingi wa magulio.

Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa