Home » » Ajali ya Fuso, 'kipanya' yaua wanane, yajeruhi 17

Ajali ya Fuso, 'kipanya' yaua wanane, yajeruhi 17



Watu wanane wamefariki dunia na wengine 17 kujeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyotokea mjini Shinyanga.


Katika ajali hiyo ambayo watu hao walifariki hapo hapo ililihusisha lori aina ya Fuso lililogongana uso kwa uso na Toyota Hiace katika barabara ya Mwanza-Shinyanga.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangalla, alisema jana kuwa ajali hiyo ilitokea juzi asubuhi katika kijiji cha Kolandoto, Manispaa ya Shinyanga.

Kamanda Mangalla alisema kuwa Hiace namba T.914 BSV iliingia barabarani bila tahadhari na kugongana na Fuso lenye namba T. 650 APS, mali ya Victor Peter.

Kamanda Mangalla alifafanua kuwa Hiace iliyokuwa na abiria ambao idadi yao haikufahamika mara moja, ilikuwa ikiendeshwa na dereva Nassibu Said (42), mkazi wa Maganzo, wilayani Kishapu likitokea Hospitali ya Kolandoto wakati likiingia katika barabara kuu ghafla liligongana uso kwa uso na lori lililokuwa likitokea mkoani Mwanza kuelekea mjini Shinyanga na kusababisha maafa hayo.

Alisema watu wanane walikufa papo hapo na kwamba saba kati yao tayari wametambuliwa, aliwataja kuwa ni Mussa Abdalah (30), mfanyabiashara wa Maganzo; Violet Wilson (51), mkazi wa Maganzo; Hussein Bakari (35), mkazi wa Maganzo na Soud Emmanuel (40), mfanyabiashara wa Maganzo.

Wengine ni Leonard Nyabwinyo (19), mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Shinyanga; Marius Benny (15), mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Shybush na Jacob Kitale (55), mwalimu wa Shule ya Sekondari Songwa.

Kamanda Mangalla alisema kuwa mtu wa nane mwenye umri kati ya miaka 12 na 14 bado hajatambuliwa jina wala makazi yake.

Mangalla aliwataja majeruhi katika ajali hiyo kuwa ni Nassibu Said (32), Benjamin John (17), Deogratius Sanyiwa na Rajabu Senema (39) ambao ni wakazi wa Maganzo pamoja na Jackson Nyabwinyo (16), mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Shinyanga.

Mareruhi wengine ni mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja, Stephen Ndaki, mkazi wa Mwadui; Silas Hosea (30), mkazi wa Masagala Maganzo; Nezeth Kiondo (45), mkazi wa Musoma mkoani Mara; Zakaria Chacha (32), mkazi wa Musoma; Gerald Helpy (14), mkazi wa Musoma na Elias Mipawa (18), mkazi wa mjini Shinyanga.

Kwa mujibu wa Mangalla, majeruhi wengine ni Bahati Mgeta (18), mkazi wa Mwanza; Sophia Njika (37), mkazi wa Wishiteleja Kishapu; Mariamu Peter (16), mkazi wa Maganzo; Rukia Hamisi (27), mwalimu wa shule ya msingi Bubiki na Shija Ndali, mkazi wa Mwadui.

Kamanda Mangalla aliwataja majeruhi wengine kuwa ni  Ranju Mnyire (19), mkazi wa Igunga mkoani Tabora na kwamba majeruhi wote wamelazwa katika Hospitali ya Kolandoto. Aliongeza kuwa hali zao zinaendelea vizuri.

Tayari polisi inawashikilia madereva wote wawili na magari yaliyohusika katika ajali hiyo yanashikiliwa katika kituo cha polisi mkoani Shinyanga.

Mangalla alifafanua kuwa baada ya uchunguzi wa kubaini chanzo halisi cha ajali hiyo madereva hao watafikishwa mahakamani kujibu mashitaka dhidi yao.

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa