Home » » NHIF KUMUENZI NYERERE KWA HUDUMA BURE

NHIF KUMUENZI NYERERE KWA HUDUMA BURE



na Mwandishi wetu, Shinyanga
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeahidi kutoa huduma za kupima afya bila malipo kwa wananchi wote siku ya kilele cha kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Akizungumzia zoezi hilo, Mkurugenzi wa Uendeshaji Eugen Mikongoti alisema NHIF imefikia uamuzi huo ili kuenzi mazuri yaliyofanywa na Baba wa Taifa enzi za uhai wake.
“Baba wa Taifa aliapa kupigana na maadui watatu ambao ni umaskini, ujinga na maradhi na katika hayo sisi ni wadau katika kupambana na maradhi ndiyo maana tumemuenzi kwa njia hii ambapo wananchi watapima afya zao bila malipo na kupata ushauri wa kitaalamu ili kuepukana na maradhi yasiyoambukiza,” alisema Mikongoti.
Mbali na upimaji, mfuko unatumia fursa hiyo kujibu kero za wanachama wake watakaofika kwenye viwanja vya sabasaba ambako NHIF imeweka banda maalumu kuendesha kwa shughuli hizo kwa siku tano kuanzia jana.
“Mfuko umehakikisha kwamba huduma za afya vituoni zinaboreka na unafanya hivyo kwa kutambua kuwa mhimili mkubwa wa Mtanzania katika kufanya kazi na kujiondolea umaskini ni afya yake kwanza… nawaomba wananchi wa Shinyanga na maeneo mengine mfike katika banda letu kupata huduma,” alisema.
Mikongoti alisema mfuko utaendelea kumuenzi Baba wa Taifa kwa kupambana na maradhi ili kuhakikisha Watanzania wanapata uhakika wa matibabu kwa kujiunga na NHIF na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
Wakati huohuo, mfuko umeendeleza jitihada za kuhakikisha makundi maalumu yanapata huduma bora baada ya kuchangia sh milioni 1.5; mashuka 80 na fulana 80 yalitolewa kwenye kituo cha Mihuji Chesire Home kilichoko mjini Dodoma kinacholea watoto wenye matatizo ya mtindio wa ubongo.
Mchango huo wa NHIF ulitolewa mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Dodoma katika harambee ya kuchangia kituo hicho na Meneja wa Kanda ya Kati Dk. Daudi Bunyinyiga aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu NHIF Emanuel Humba.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa