Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe.Ally N. Rufunga |
Serikali Mkoa Shinyanga imeondoa baadhi ya michango
inayotozwa katika shule za Sekondari ambayo imekuwa kero na mzigo kwa wazazi, hasa
mwanafunzi anapoanza kidato cha kwanza.
Maamuzi hayo yamefikiwa katika kikao cha Wadau wa Elimu
kilichofanyika jana chini ya Mwenyekiti wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga
Mheshimiwa Ally Nasoro Rufunga ambacho kiliwahusisha wadau mbalimbali wa Elimu
ndani ya Mkoa kuanzia wanafunzi, wazazi, walimu,viongozi wa serikali,wataalamu
wa Elimu na viongozi wa vyama vya siasa,asasi za serikali na binafsi.
Michango hiyo imeondolewa baada ya wazazi wengi kutoa
malalamiko kwa Mkuu wa Mkoa kuwa, kumekuwa na michango mingi mbali na karo, ambayo
wazazi wanashindwa kumudu gharama hivyo kushindwa kupeleka watoto wao shule kwa
wakati kwa sababu wazazi wengi wana kipato cha chini.
Michango iliyoondolewa ni pamoja na michango ya
Majengo,masweta na sare za shule.
Mkuu wa Mkoa alikieleza kikao kuwa, pamoja na maamuzi hayo,
serikali itapeleka maelekezo katika bodi na kamati za shule ziwasilishe Mkoani
aina yoyote ya michango iliyokubalika katika vikao vya bodi na kamati hizo ili
Mkoa uidhinishe michango hiyo kama ina umuhimu.
Aidha,katika kikao hicho serikali ya mkoa wa Shinyanga
imeazimia kuboresha Elimu katika mkoa huu kwa kuanza kufanyia kazi baadhi ya
changamoto na kisha kufanya tathmini baada ya mwaka mmoja kwa lengo la kumaliza
tatizo moja baada ya lingine.
Changamoto zilizopewa kipaumbele ni Kuhakikisha wanafunzi
wanapata chakula shuleni, kuongeza idadi ya walimu hasa maeneo ya vijijini na kuimarisha
idara ya ukaguzi wa shule, pia, kukamilisha idadi ya madawati ya kutosha,
kuthibiti utoro na mimba kwa kuwachukulia hatua kali za kisheria wanaosababisha
utoro kwa wanafunzi na wanaowapa mimba pamoja na kuongeza motisha kwa walimu
waajiriwa wapya wanaoripoti.
Mkuu wa Mkoa pia amewazawadia wanafunzi waliofanya vizuri
katika ngazi ya mkoa katika mitihani ya Mwaka jana 2012 darasa la saba, kidato
cha nne na kidato cha sita pamoja walimu wao waliofanyan vizuri.
Akifunga kikao hicho amewataka wadau wote kusimamia sheria
zilizopo kwa kila mmoja kuwajibika katika sehemu yake, hususani Maafisa Elimu
wa Wilaya amewataka wasifanye kazi kwa mazoea.
0 comments:
Post a Comment