VIONGOZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wametakiwa kuzungumza mafanikio yaliyofikiwa na chama hicho na kutambua uimara wake kwa jamii. Hayo yalisemwa juzi na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja katika kikao cha ndani kilichojumuisha wanachama, mabalozi, wazee, pamoja na wajumbe wa halmashauri kuu ya kata ya Kilago wilayani Kahama.
Alisema hivi sasa chama hicho, kinakabiliwa na tatizo la baadhi ya viongozi wa chama kutozungumzia mafanikio ya chama ambayo yamepatikana na kuwaachia wapinzani kutamba.
“Hii ni kasoro kubwa ndani ya chama, wapinzani wanatutukana na kuitwa jembe! Jembe gani hilo kama sio jembe la matusi,” Mgeja alisema.
Aliwataka viongozi kutimiza wajibu wao wa kusimamia ilani yake, hali ambayo itasaidia suala zima la kuimarisha chama hicho ambacho kinapendwa na kinazidi kupendwa na kuaminiwa na wananchi kila kukicha.
Katika hatua nyingine, aliwaomba wana CCM kuacha tabia ya kugombania madaraka, kuchukiana na kusengenyana na kuongeza kuwa uchu wa vyeo pamoja na madaraka katika chama hicho ndio sababu inayochangia kupoteza mshikamano ndani ya Chama Cha Mapinduzi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti mstaafu wa CCM Wilaya ya Kahama, Edward Msoma, alisema anasikitishwa na ugomvi ambao umekuwa ukitokea ndani ya CCM.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Ufala, wanachama wapya 310 walijiunga na CCM wakitoka vyama vya upinzani.
Katika hatua nyingine, Mgeja alichangia mifuko 20 ya saruji pamoja na matofali 3000, mjumbe wa NEC, Dk. Catherine Dalali alichangia mifuko miwili ya saruji na Diwani wa Kata ya Ilemela, wilayani Chato, Ismail Ruge alitoa mifuko 10.
CHANZO: MTANZANIA
0 comments:
Post a Comment