Hakimu wa Mahakama ya
Mwanzo iliyopo eneo la Nguzo Nane, Kata ya Kambarage Mjini Shinyanga, Satto
Nyangoha amejeruhiwa kwa kuchomwa kisu katika shavu lake la kushoto baada ya
kutoa hukumu ya kesi ya wizi wa baiskeli.
Wauguzi wa
hospitali ya mkoa wa Shinyanga wakimuhudumia hakimu Satto Nyangoha aliyechomwa
kisu shavuni jana, akiwa mahakamani na mlalamikaji katika kesi ya wizi wa
baiskeli, Emmanuel Izengo. Picha na Suzy Butondo
Kitendo hicho kinadaiwa kufanywa na mlalamikaji
katika kesi hiyo, Emmanuel Izengo (28), mkazi wa Tambukareli, Shinyanga baada
ya kutokuridhishwa na hukumu iliyotolewa bila ya mshtakiwa, Daniel Makelezia,
mkazi wa Lubaga Shinyanga na mdhamini wake, Marko Nkelezia kuwepo mahakamani.
Katika hukumu yake, Hakimu Nyangoha alisema
mshtakiwa atakapopatikana atatumikia kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana
na hatia ya wizi wa baiskeli hiyo aina ya Neria yenye thamani ya Sh150,000.
Awali, ilielezwa kwamba baada ya tukio hilo la
wizi lililotokea Agosti Mosi, mwaka huu katika eneo la Nguzo Nane, mshtakiwa
alikamatwa na kuwekwa mahabusu na kufunguliwa kesi namba 460 ya 2013 kabla ya
kuachiwa kwa dhamana Agosti 23, mwaka huu huku kesi yake ikiendelea na pande
zote mbili zilitoa maelezo.
Hata hivyo, baada ya kutoa maelezo, si mshtakiwa
wala mdhamini wake aliyehudhuria mahakamani hapo licha ya kesi hiyo kusikilizwa
mara mbili bila ya taarifa yoyote kabla ya hakimu huyo kutoa hukumu hiyo jana.
Kushambuliwa
Baada ya hukumu hiyo mlalamikaji alitoa shukrani
na kuwashika mikono wote waliokuwamo mahakamani humo na kutoka nje.
Ilidaiwa kuwa baada ya dakika 15, Izengo alirudi
mahakamani hapo na kudai kuwa ameleta risiti ya kumwonyesha hakimu thamani ya
baiskeli yake alipoingia ndani ndipo kelele za Mshauri wa Baraza, Mary Wamba
zikaanza kusikika akisema: ‘Njooni jamani hakimu kavamiwa anapigwa’.
Baada ya watu waliokuwa karibu kuingia katika
ofisi ya Mahakama hiyo walikuta hakimu ameshacwhomwa kisu katika shavu la
upande wa kushoto huku akivuja damu nyingi huku mtuhumiwa huyo akiendelea
kumshambulia. Baada ya tukio hilo, wasamaria wema walimpeleka hakimu huyo
katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga ambako alilazwa kwa matibabu.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Shinyanga, Evarist Mangala alisema mtuhumiwa alikamatwa mara baada ya tukio
hilo kusubiri hatua za kisheria dhidi yake.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment