MKUTANO wa kujadili Rasimu ya Katiba Mpya
ulioandaliwa na Chama cha Wasioona wilayani Kahama umevunjika baada ya
washiriki kususia wakidai posho.
Mkutano huo ulivunjika siku ya pili baada ya
wajumbe hao kutoka asasi mbalimbali zisizokuwa za kiserikali wakiongozwa na
baadhi kutoka kwa Chama cha Walemavu wa Macho na Viungo, kukataa kuhudhuria
mkutano huo hadi Ofisa wa Ruzuku wa The Civil for Foundation Society, Ghati
Horombe, kutangaza kuwalipa posho hizo.
Tangazo la ofisa huyo liliongeza idadi ya washiriki
kwa siku ya tatu jambo lililomfanya Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu
wenye Ulemavu wilayani Kahama, Maico Nkanjiwa aliwaonya kuacha tabia ya
kutanguliza maslahi katika masuala ya kujadili maisha yao.
Siku ya kwanza wajumbe zaidi ya 100 walihudhuria
baada ya Nkanjiwa kuwatangazia kuwa kusingelikuwa na posho isipokuwa
wangelipata chai na chakula cha mchana; jambo hilo lilizusha mzozo kwa
washiriki hao wakidai wasingeliwezi kushindia chakula.
Walisema wasingeliweza kula chakula huku familia
zao zikiadhirika kwa kushinda na njaa majumbani mwao na kudai kuwa ni vema
wangeondoa gharama za chakula, badala yake kuwalipa pesa, kuliko kuwashindisha
hapo bila malipo.
Kwa upande wake Horombe aliwataka Watanzania kuacha
tabia hiyo kwa kuwa inaleta sura mbaya kwa wafadhili.
Hata hivyo mkutano huo ulimalizika kwa washiriki
kuunga mkono uwepo wa serikali tatu kwa madai kwamba serikali mbili haina
maslahi kwa Watanzania.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment