JESHI la Polisi mkoani Shinyanga limetoa zawadi kwa wananchi pamoja
na Sungungu katika kata za Segese na Lunguya, wilayani Kahama baada ya
kufanikisha kukamatwa kwa watu watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi
yakiwa na silaha aina ya SMG na risasi 26.
Kaimu Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi, Kihenya
Kihenya, alisema jana kuwa Sungusungu na wananchi hao walifanikisha
kukamatwa kwa watuhumiwa watatu ambao wanasadikiwa kufanya uhalifu wa
kuvamia maduka matatu na kufanikiwa kupora sh 180,000 na vocha za simu.
Kihenya alisema watuhumiwa hao waliteka maduka hayo saa mbili usiku na
baada ya kufanya uhalifu huo walitoweka na kuelekea katika kijiji cha
Segese, lakini wananchi hao kwa kushirikiana na Sungusungu pamoja na
polisi walifanikiwa kuwakamata.
Alisema wananchi walikamata bunduki hiyo na risasi hizo nyumbani kwa
mtuhumiwa, Amoni Lubisi (24) ikiwa imehifadhiwa kitandani chini ya
godoro pamoja na risasi zake.
Pia wananchi hao waliwakamata watuhumiwa wote watatu: Amoni Lubisi na
kaka yake Silasi Lubisi (25) pamoja na Bakari Ramadhan (32) wote wakiwa
wakazi wa Segese kilometa chache kufika Lunguya eneo walilokwenda
kufanya uhalifu huo.
Polisi Shinyanga imetoa sh 100,000 iliyokabidhiwa kwenye kata hizo
mbili na Kamanda Kihenya ambapo Kamishina Msaidizi Mwandamizi kutoka
Makao Makuu ya Upelelezi wa Jeshi hilo nchini alitoa sh 50,000 pamoja na
Kamishna Msaidizi kutoka Makao Makuu hayo, Mohamed Salim naye alitoa sh
80,000.
Naye Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kahama, Mrakibu Mwandamizi William
Mlekwa, alitoa sh 50,000 huku akiwataka wananchi hao kutekeleza falsafa
mpya ya Polisi ya ‘Familia Yetu Haina Mhalifu’ hali itakayosaidia
kutokomeza uhalifu na mauaji ya vikongwe
Chanzo;Tanzania daima
0 comments:
Post a Comment