Home » » ‘Acheni kufanya biashara za kuigana’

‘Acheni kufanya biashara za kuigana’

Shinyanga. Mratibu wa Mafunzo ya Ujasiriamali kutoka Shirika la Alied Kemiko, Debora Magese amewataka wajasiriamali nchini kuwa wabunifu na kuepuka kufanya biashara za kufanana ili kukuza kipato chao.
Hayo aliyasema jana wakati akifungua mafunzo yaliyoshirikisha wajasiriamali wa Mjini Shinyanga. Magese alisema kuwa wafanyabiashara wengi hufanya biashara ya kufanana hali ambayo hufanya kugombania wateja.
Magese alisema asilimia kubwa ya wafanyabiashara hufanya biashara za kufanana sehemu moja kutokana na wengi wao kukosa elimu ya ujasiriamali ya kuendesha biashara hizo na kushindwa kufanya utafiti wa biashara.
“Wafanyabiashara wengi hapa nchini hufanya biashara za kuigana kutokana na kukosa elimu ya ujasiriamali, ambayo ingeongezea jinsi ya kufanya utafiti wa kuvumbua biashara ambayo itawainua kiuchumi na siyo kufanya biashara za aina moja za kunyang’anyana wateja” alisema Magese.
“Mtu mmoja akianza kufanya biashara fulani na kufanikiwa, mwingine nanye anaanzisha biashara kama hiyo tena eneo moja, hii siyo sahihi. Tuwe wabunifu.”
Aliongeza kuwa wao kama shirika, wameamua kutoa mafunzo hayo kwa wafanyabiashara pamoja na wananchi wa kawaida kwa lengo la kupunguza idadi ya watu wasio na ajira. Alisema mbali na kutoa elimu ya ujasiriamali, wanatoa ujuzi wa kutengeneza bidhaa mbalimbali kama vile kutengeneza Dawa za Chooni, Batiki, Mafuta ya Mgando na sabuni za kufulia.
Semina hiyo ya wajasrliamali ilianza jana mjini Shinyanga katika Ukumbi wa Shirika la Viwanda Vidogo (Sido) na inatarajiwa kumalizika Desemba 14.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa