WAZAZI wametakiwa kushirikiana na mashirika ya kijamii yanayoendesha
miradi mbalimbali ikiwemo ya kuwaendeleza watoto wa kike walioacha
masomo kwa kuhakikisha wanawaruhusu kushiriki kwenye miradi
itakayowakwamua kimaisha.
Rai hiyo ilitolewa na Makamu Mweyekiti wa Halmashauri ya Msalala
wilayani Kahama, Shinyanga, Benedict Manwari, katika kikao
kilichoandaliwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Kiota Women
Health Development (Kiwohede) na kuhudhuriwa na wazazi pamoja na
viongozi wa kata ya Lunguya.
Manwari alisema jamii imekuwa haiamini mashirika yanayoendesha miradi
yake hali inayosababisha baadhi yao kushindwa kuwaruhusu watoto wao
kujiunga na kushiriki.
Pia aliwataka wazazi kushirikiana na mashirika hayo ikiwemo shirika la
Kiwohede ambalo linaendesha mradi wa afya ya uzazi na kuwajengea uwezo
wa kujiajiri na kuwa wajasiriamali wasichana wenye umri kati ya miaka 10
hadi 19 ambao walikatisha masomo kutokana na kuolewa katika umri mdogo
na kupata mimba za utotoni.
Mkurugenzi wa Kiwohede, Justa Mwaituka, alisema shirika hilo limelenga
kuwasaidia wasichana hao kwa kuhakikisha wanarudishwa shule kwa wale
watakaohitaji na wengine kuwapatia mafunzo ya ufundi stadi wa fani
mbalimbali ili kuwajengea uwezo wa kujitegemea.
Mwaituka alisema malengo ya mradi huo ni kuwezesha wasichana 60 katika
fani mbalimbali ambapo shirika limelenga kuwafikia wasichana wengi
katika kata za Lunguya, Shilela, Busoka na Mhongolo watakaopata mafunzo
kupitia vituo vilivyotengwa.
Alisema kwa awamu ya kwanza wasichana 60 watapelekwa katika Chuo cha
Maarifa ya Nyumbani cha Mwanva ambao watasoma kulingana na fani
watakayoichagua kwa kulipiwa gharama zote na Kiwohede kwa miezi sita.
Chanzo;Tanzania daima
0 comments:
Post a Comment