Home » » Halmashauri Ushetu yapitisha bajeti bil. 32/-

Halmashauri Ushetu yapitisha bajeti bil. 32/-

Mkurugenzi Mtendaji, Isabela ChilumbaBARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Ushetu katika Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga limepitisha mapendekezo ya mpango wa bajeti ya sh bilioni 32.5 kwa mwaka wa fedha 2014/2015.

Akisoma mapendekezo ya mpango wa bajeti wa mwaka  2014/2015, Mkurugenzi Mtendaji, Isabela Chilumba, alisema kiasi hicho cha fedha wanatarajia kukitumia katika shughuli mbalimbali za maendeleo sambamba na mishahara  ya watumishi.
Chilumba alisema matumizi katika bajeti hiyo ni sh bilioni 30.7 ambazo zitatokana na ruzuku kutoka Serikali Kuu, huku shilingi bilioni 1.8 ni kutoka katika vyanzo vyake vya mapato ya ndani ikiwa ni pamoja na sh bilioni 1.1 kutoka ushuru wa zao la tumbaku.
Hata hivyo, Isabela alisema katika bajeti ya mwaka 2013/14 halmashauri yake ilikadiria kukusanya shilingi bilioni 39.3, ikiwa ni sh bilioni 37 ruzuku ya serikali, huku mapato ya ndani ikiwa ni sh bilioni 2.3.
Akifafanua zaidi Chilumba alisema bajeti hiyo mwaka huu imeshuka kutokana na kujitenga kwa Halmashauri ya Msalala, ambayo nayo imeandaa bajeti yake kwa kujitegemea tofauti na mwaka huo ambapo zilikuwa pamoja.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Juma Kimisha, alisema changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa miradi ni ucheleweshwaji wa ruzuku kutoka serikalini, ambayo hufika kwa kusuasua na pengine kutofika kabisa, hali inayofanya baadhi ya miradi kutokamilika.
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa