JESHI
la polisi mkoa wa Singida linawashikilia watu 15 kwa tuhuma za kuchoma
moto basi la kampuni ya Mtei, baada ya kuwagonga wapanda pikipiki na
kusababisha vifo vya wanafamilia watatu.
Kamanda wa polisi Mkoa
wa Singida Geofrey Kamwela amesema kuwa watuhumiwa hao wanaendelea
kuhojiwa kwa kosa la kulisababishia uharibifu basi hilo lenye namba za
usajili T 742 ACU aina ya Scania lililokuwa likiendeshwa na Disma Ludovik
kutoka Singida kwenda Arusha.
Baada ya kufika eneo la Januka nje kidogo ya Mji
wa Singida Januari 09, mwaka huu, basi hilo liligonga
Pikipiki yenye namba T.368 BXZ Skygo, iliyokuwa imepakiwa watu
wanne na kusababisha vifo vya watatu kati yao.
Kamanda Kamwela amesema
baada ya wanafamilia hao kufa na baba yao mzazi aliyekuwa dereva wa pikipiki
kulazwa Hospitali ya Haydomb Mbulu kwa matibabu hadi sasa, watuhumiwa
walijichulia sheria mkononi kwa kuchoma basi hilo na kusababisha
hasara ya zaidi ya shilingi milioni 70.
Kamanda Kamwela amesema
watuhumiwa hao 15 akiwemo diwani wa kata ya Unyambwa Shabani
Satu wanatarajiwa kupandishwa kizimbani wakati wowote kujibu shitaka
linalowakabili.
0 comments:
Post a Comment