Kaliua. Wachimbaji wa madini katika Kijiji cha Nsungwa kwenye
machimbo ya dhahabu wamepigwa marufuku kulipua miamba kwa kutumia baruti
wakati wa usiku.
Akizungumza kwenye kikao na wachimbaji wa madini,
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua, Ibrahim Kifoka
alisema ulipuaji miamba wakati wa usiku ni kinyume cha sheria kwa vile
sheria imeweka mwisho kuwa saa kumi na mbili jioni.
“Ulipuaji miamba kwa mujibu wa sheria mwisho ni majira ya saa kumi na mbili jioni na sio baada ya muda huo,” alisema.
Alieleza kwamba hatua hiyo imetokana na malalamiko
ya wananchi kuwa baadhi ya wachimbaji wamekuwa wakilipua miamba kwa
ajili ya madini hadi usiku wa manane jambo ambalo halikubaliki. Aliweka
bayana kuwa ulipuaji huo nyakati za usiku,umesababisha watu kupata
shinikizo la moyo na kushindwa kulala hali amabayo imekuwa ikiwaletea
usumbufu mkubwa.
Awali wachimbaji wadogo walieleza kilio chao kuwa
wamekuwa wakitakiwa kutoa mgawo kwa wamiliki wawili wa machimbo ya
dhahabu badala ya mmoja.
Walieleza kuwa wamiliki hao Seleman Mihambo na
Mohamed Lasweed, wamekuwa wakidaiwa mgawo wa machimbo yao kutoka kwa
wachimbaji wadogo, ambao wamekuwa hawajui wampe nani..
Akitolea uamuzi jambo hilo, Kifoka aliwataka
wamiliki hao wasichukue mgawo kutoka kwa wachimbaji hadi maofisa wa
madini toka Tabora watakapotatua tatizo hilo.
Ili kuwa na usalama kwenye eneo hilo,iliamuliwa
katika kikao hicho kuchaguliwa wakaguzi wa usalama ambapo walichaguliwa
Omary Salum na Jaffary Mtima.
Machimbo ya Madini ya Dhahabu ya Nsungwa katika
Kata ya Silambo wilayani Kaliua yanatoa dhahabu ambapo wachimbaji wadogo
wanatumia eneo hilo kuchimba dhahabu huku wakitoa mgao kwa wamiliki wa
eneo hilo.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment