Home » » Wafuasi wa Zitto wadhibitiwa mkutano wa Chadema

Wafuasi wa Zitto wadhibitiwa mkutano wa Chadema

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe.
 
Vijana watatu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe, juzi walijikuta katika wakati mgumu baada ya mabango waliyokuwa wamebeba katika mapokezi ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, kuchanwa na wananchi mjini Shinyanga.
Dk. Slaa na viongozi wengine waandamizi walikuwa na ziara ya kuhutubia mikutano ya Operesheni M4C “Pamoja Daima”.

Tukio hilo lilitokea muda mfupi baada ya msafara wa Dk. Slaa kushuka kutoka kwenye helikopta iliyotua katika uwanja wa ShyCom  kwa ajili ya mkutano wa hadhara.

Vijana watatu waliokuwa wamebeba mabango waliyaelekeza kwa Dk. Slaa aliyeongozana na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, John Mnyika na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Said Issa Mohamed, yakisomeka “Zitto yuko wapi?” na “Zitto mnamuonea.”

Baada ya viongozi hao kusoma mabango hayo Mnyika alimhoji mmoja wa vijana waliokuwa wameyabeba kama anamfahamu Zitto, lakini kijana huyo alijibu anamfahamu kwa kumuona kupitia kwenye runinga  tu na kwamba hajawahi kukutana naye uso kwa uso.

Kufuatia hali hiyo, wananchi waliokuwa katika mkutano huo waliwazomea vijana hao na  kuyachana mabango yote waliyokuwa nayo.

Baada ya Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Magharibi, Sylivester Kasulumbai, kumkaribisha Mnyika kuwahutubia wananchi, mbunge huyo wa Ubungo alieleza jinsi yeye na Zitto walivyojiunga Chadema na kufafanua sababu zilizosababisha Zitto achukuliwe hatua za kinidhamu kwa kuvuliwa nyadhifa zake za uongozi na Kamati Kuu kwa mujibu wa katiba ya chama.

Alisema katiba inaeleza kuwa kiongozi  atakayekiuka maadili atasimamishwa au kufukuzwa uanachama na kusema Zitto alikiuka maadili ya chama na kwamba hatma ya uanachama wake kwa  sasa iko mahakamani.

Kwa upande wake,  Dk. Slaa alisema mwanachama anayejiunga na chama kwa kumfuata mtu fulani huyo hajui siasa.

Dk. Slaa alisema: “Kama kuna mtu anamuona Zitto ndiye Chadema basi amfuate yeye,  sisi chama chetu hakina kizuizi ruksa kuungana naye.”

Naye, Mohamed alitumia baadhi ya  vifungu vya Koran akieleza kuwa alipokufa Mtume Mohamad, wafuasi wake walibaki na hawakumfuata na kama mtu anamuona Zitto anafaa kwake amfuate.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa