Home » » CHADEMA: Uwekezaji umegubikwa na uporaji rasilimali

CHADEMA: Uwekezaji umegubikwa na uporaji rasilimali

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kutokana na uongozi mbovu na sera zisizomlinda Mtanzania, uwekezaji katika madini umegubikwa na uporaji mkubwa wa rasilimali na tayari nchi imeanza kuachiwa mashimo.
Chama hicho kimesema kuna njia mbili pekee za kuwanusuru Watanzania, pamoja na kuliokoa taifa kuondokana na ufisadi na uporaji wa rasilimali za nchi, ambayo ni wananchi kuwabana wabunge na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuhakikisha Katiba mpya inakuwa na ibara inayozingatia haki za wananchi kumiliki na kunufaika na rasilimali.
Akizungumza katika mfululizo wa mikutano ya Mpango wa M4C- Operesheni Pamoja Daima katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Shinyanga juzi na jana katika maeneo ya Msalala (Kakola), Kahama mjini, Shinyanga mjini, Iselamagazi, Kishapu, Mhunze, Itilima (Lugulu), Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mahusiano wa CHADEMA, John Mnyika, alisema mgodi wa Bulyag’hulu ulianza uzalishaji mwaka 2001 na tayari hadi sasa umetoa tani za ‘ounce’ (toz) milioni 3.29 huku serikali ikiwa imelipwa sh bilioni 337 pekee.
Alisema Watanzania wanashindwa kunufaika na rasilimali zao kwa sababu ya katiba, sheria na mikataba mibovu iliyoingiwa chini ya CCM kama chama kilichoko madarakani kwa sasa.
Akiwa Shinyanga mjini, Mnyika ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, alikumbusha kwamba ilani ya uchaguzi ya CHADEMA ya mwaka 2005 iliweka mkazo katika kutetea rasilimali za nchi ikiwemo madini, kashfa za Richmond, Buzwagi na EPA zilipoibuka bungeni CHADEMA ilikodi helikopta na kuwazungusha viongozi wa vyama na wabunge, kupeleka hoja kwa wananchi.
“Operesheni hiyo ilianzia kwa mapokezi Dar es Salaam na iliishia Septemba 15, 2007 Mwembeyanga ambapo orodha ya mafisadi ilisomwa. Hatua hiyo ilimsukuma Rais Kikwete kuunda Kamati ya Bomani kuhusu madini, Kamati ya IGP kuhusu EPA na Bunge likaunda Kamati Teule kuhusu Richmond.
“Sasa tunawashangaa wanafiki na wasaliti ambao wanafanya mikutano ya hadhara kubeza hatua hiyo ya CHADEMA ya wakati huo ambayo ilifungua ukurasa mpya katika mapambano dhidi ya ufisadi na utetezi wa rasilimali nchini.
“Kwa hiyo mbinu ya kwanza ni hiyo kuwabana kabisa wabunge na wajumbe wa Bunge la Katiba, ili kifungu cha haki za rasilimali kiingizwe kwenye Katiba Mpya. Mbinu ya pili ni kuiondoa serikali madarakani na kuichagua CHADEMA katika chaguzi zote zinazokuja, ili kupata uongozi bora na sera sahihi, masuala ambayo hayawezi kutekelezwa na CCM iliyoshiriki kuingia mikataba mibovu,” alisema Mnyika.
Kwa upande wa Mgodi wa Buzwagi, Mnyika alisema tayari kuna kasi kubwa ya uchimbaji wa dhahabu ambapo tangu mwaka 2009 hadi sasa tani za aunzi (toz) milioni moja  za madini huku mapato kwa serikali yakiwa ni sh bilioni 74 pekee, ambapo pia sehemu kubwa ikiwa ni makato ya wafanyakazi wanaokatwa kodi lukuki.
Mnyika alisema mgodi huo ambao umeanza uzalishaji miaka ya karibuni, unafikia ukomo miaka 6 ijayo kutokana na kasi ya uchimbaji, hivyo akawataka wananchi kuiondoa CCM haraka madarakani, ili walau kuokoa migodi kama Bulyag’hulu ambao bado una miaka 21 na ule wa almasi wa Mwadui ambao umebakiza miaka 14.
“Kutokana na mikataba mibovu, sheria na sera mbovu za madini, tayari kuna migodi mikubwa ambayo taifa limeanza kuachiwa mashimo na mfano mzuri kabisa ni jirani tu hapo kwenye Mgodi wa Nzega uliokuwa chini ya Kampuni ya Golden Pride, Mgodi wa Tulawaka, Biharamulo uliokuwa chini ya African Barrick Gold. Kote huko tumeachiwa mashimo, wananchi na nchi bado maskini, utajiri umeondoka,” alisema Mnyika.
Alibainisha pia kuwa umefika wakati ili kuyabana makampuni ya madini, wafanyakazi wa migodini kuwa na nambari maalumu za mlipakodi (Tin), ili mchango wao wa malipo ya serikali ubainike badala ya sasa ambapo huingizwa kwenye kapu moja la malipo ya kampuni.
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa