IMEELEZWA wanaume wanaongoza kwa kutopima virusi vya ukimwi (VVU)
kutokana na kutawaliwa na hofu inayosababishwa na kumiliki ‘nyumba
ndogo’ nyingi huku wakiwa wahamasishaji wazuri kwa wake na wapenzi wao
kutambua afya zao.
Hayo yalielezwa na Mkufunzi Mkuu wa Kitengo cha Ukimwi kutoka
hospitali ya mji wa Kahama, Ofisa Muuguzi, Emerenciana Machibya, katika
semina ya kujitambua na kupata elimu ya ugonjwa huo iliyowahusisha
wanaume kutoka migodini na madereva wa magari makubwa wilayani Kahama.
Katika semina hiyo iliyoendeshwa na shirika lisilo la kiserikali la
The Foundation for Human Healthy Society (Huheso Foundation) la
wilayani Kahama, Machibya alisema wanaume wengi hawapendi kutambua
afya zao kwa kupima na badala yake huwasukuma wake zao kwenda
hospitali peke yao kama chambo.
“Kinababa wa ajabu sana, kwani hushindwa kuwasindikiza wake zao
kliniki wanapokuwa wajawazito, hubakia wakisikilizia majibu ya vipimo
kutoka kwa wake zao ambao pindi wakiwa hawana virusi basi nao
hujiaminisha kuwa wapo salama, jambo ambalo si kweli,” alisema
Machibya.
Alisema pamoja na tafiti kuonyesha wanawake ndio wanaongoza kwa
kujitokeza kupima, lakini pia wanaongoza katika maambukizi, ambapo
alisisitiza umuhimu kwa jamii kuchunguza afya zao mara kwa mara.
Ofisa Muuguzi Mkuu katika Halmashauri ya Mji, Richard Kajogo,
aliwataka wanaume kuwa jasiri kwa kujitokeza kupima, ili
wanapogundulika wapate huduma za afya.
Mkurugenzi wa Huheso Foundation, Juma Mwesigwa ambaye shirika lake
limefadhiliwa na RFE ya jijini Dar es Salaam kutekeleza mradi wa
kuwakomboa wanawake na wasichana katika biashara ya ngono, alisema ili
kukabiliana na janga hilo ni vema wanaume kuondokana na mfumo dume wa
maisha
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment