HALMASHAURI
ya Wilaya ya Kishapu Mkoa wa Shinyanga imepanga kutumia kiasi cha
sh.91,200,000 kwa ajili ya utekelezaji mpango kabambe wa kusaidia
kubadilisha uchumi na hali ya maisha ya wafugaji katika wilaya hiyo.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa wiki iliyopita na Mkuu wa Wilaya ya
Kishapu Wilson Nkhambaku kwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi
nchini, Dkt. Titus Kamani miongoni mwa shughuli zitakazotekelezwa
kupitia fedha hizo ni ununuzi wa madume bora ya ng'ombe aina ya Mpwapwa
na Borani.
Nkhambaku alisema wilaya imechukua hatua hiyo baada ya
kubaini kuwepo kwa ongezeko la mifugo isiyo ya tija ya kutosha ambayo
haiwezi kuwasaidia wafugaji kubadilisha hali za maisha yao na
kuwaongezea kipato cha kutosha.
"Tayari suala la uboreshaji wa
mifugo kwa kutumia madume bora limeonekana kupokewa kwa mwitikio mkubwa
na wafugaji katika wilaya yetu ambapo kwa mwaka 2012 wilaya kwa
kushirikiana na wafugaji iliweza kuhimilisha ng'ombe 200 katika vijiji
vinne,"
"Vijiji hivyo ni pamoja na Mwamalasa, Somagedi, Songwa na
Migunga ambako wafugaji walifanikiwa kupata ndama 15 sawa na asilimia
7.5 ya lengo tulilokuwa tumekusudia, lakini pia kwa mwaka 2012/2013
wilaya iliweza kununua madume bora 18 na kuyasambaza kwa wafugaji katika
vijiji vitano," alieleza Nkhambaku.
Akifafanua mkuu huyo wa wilaya
alisema katika mwaka wa fedha wa 2013/2014 wilaya imetenga jumla ya
shilingi 16,200,000 kwa ajili ya ununuzi wa madume bora 18 na mwaka
2014/2015 jumla ya shilingi 71,000,000 zitatumika kununulia madume bora
100 aina ya Mpwapwa na Borani yatakayosambazwa kwa wafugaji.
Nkhambaku
alisema kiasi cha sh.4,000,000 kimetengwa kwa ajili ya shughuli ya
uhamilishaji na kwamba matarajio ya wilaya hiyo ni kuendelea
kushirikiana na wafugaji ili waweze kufuga kitaalamu na hivyo kuongeza
tija katika mifugo yao.
Kwa upande wake Dkt.Kamani aliupongeza
uongozi wa Wilaya ya Kishapu kwa jinsi ulivyoonesha ushirikiano katika
utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo ikiwemo suala la
kuwasaidia wafugaji waweze kupata mifugo bora itakayokuwa na thamani
kubwa katika masoko.
"Ninakupongezeni kwa ushirikiano niliouona,
hali hii itawasaidia zaidi wananchi wetu katika utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao, hili suala la kuwasaidia
wafugaji wetu waweze kufuga kitaalamu na kuwa mifugo bora ni moja ya
vipaumbele vyangu tangu nilipokabidhiwa wizara hii,"
"Ni aibu kuona
zaidi ya miaka 50 ya uhuru wafugaji bado wanachunga ovyo, hawafugi
kitaalamu, lazima tuwasaidie kwa kuwapa elimu ya kutosha ili wanufaike
na ufugaji wao, na itapunguza kwa kiasi kikubwa migogoro iliyopo hivi
sasa kati yao na wakulima, tuwatengee maeneo rasmi kwa ajili ya ufugaji
tu," alisema Dkt. Kamani.
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment