Home » » Mgeja atamba CCM ipo imara hakuna wa kuiyumbisha

Mgeja atamba CCM ipo imara hakuna wa kuiyumbisha

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja amesema chama hicho kiko imara na kitaendelea hakuna mtu yeyote ndani na nje wa kukiyumbisha.
Akifunga kampeni za uchaguzi wa udiwani kwa nyakati tofauti vijiji vya Nonwe na Salawe, Kata ya Ubagwe, wilayani Kahama juzi, Mgeja alisema CCM inaheshimika na itaendelea kuwa imara.
Mgeja aliwataka  Watanzania kuachana na propaganda na kutoyumbishwa na watu wasioitakia mema nchi, wanaokitabia kifo chama hicho.
Alisema ndoto hizo za mchana hazina ubashiri wowote, bali CCM ikpo imara na kitaendelea kuwa imara kwani kinafanya vizuri  katika ngazi zote. CCM imemsimamisha Khamis Majogoro Mbogola kwenye uchaguzi huo mdogo uliofanyika.
“Hivyo kitaendelea kuwa imara  na hakuna mtu yeyote ndani na nje ya chama atakayekiyumbisha,” alitamba Mgeja.
Alisema chama hicho na jumuiya zake zinafanya kazi vizuri kusimamia ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2010 hadi  2015, chini ya Mwenyekiti wake,  Jakaya  Kikwete.
 Mgeja alikumbusha maneno ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere kuwa, ili maendeleo yapatikane vinahitajika vitu vitatu; Watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora ambavyo vinapatikana CCM.
 “Ndiyo kazi na malengo tangu tunadai na uhuru wetu hadi sasa, CCM na Serikali yake vinasimamia misingi hiyo vizuri japo kuna watu wachache wanafanya kwa maslahi yao, wala CCM haijawatuma,” alisema Mgeja.
 Pia, aliwaomba wananchi kuichagua  CCM  kwani ndicho chama pekee ambacho ni mwarobaini wa kutatua matatizo yao.
 “Nawaomba mpime tofauti yetu na vyama vya upinzani hasa Chadema, CCM inahubiri amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, wakati wenzatu walishaapa nchi haitatawalika nyinyi ni mashahidi na mnayaona matukio mbalimbali ya vurugu yanayofanywa nchni,”alisema Mgeja
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa