MAUAJI
ya kikatili dhidi ya wanawake wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga
yamezidi kupamba moto kufuatia tukio la kuuawa mama na mwanaye
walioshambuliwa kwa kukatwakatwa mapanga huko katika Kijiji cha Ngokolo
Kata ya Bukomela usiku wa kuamkia juzi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Shinyanga, Evarist Mangala aliwataja wanawake waliouawa kuwa ni Mhulu
Nh'ambo (50) na mwanaye Helena Charles (30), walioshambuliwa kwa
kukatwakatwa mapanga na watu wasiojulikana mnamo saa moja usiku
walipokuwa wakiandaa chakula cha usiku nyumbani kwao.
Kamanda
Mangala alisema, siku hiyo ya tukio wakati mama huyo akiwa na mwanaye
wakiandaa chakula cha usiku ghafla walivamiwa na kundi la watu
wasiojulikana ambao waliwashambulia kwa kuwakatakata mapanga sehemu za
kichwani na mgongoni hali iliyosababisha wapoteze maisha papo hapo
kutokana na kuvuja damu nyingi.
Hata hivyo, alisema chanzo cha
mauaji hayo mpaka sasa hakijafahamika na tayari polisi inamshikilia
mtuhumiwa mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi
na juhudi za kuwasaka watuhumiwa wengine zinaendelea ili waweze
kukamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu shtaka la mauaji.
Kamanda
Mangala ametoa wito kwa raia wema kutoa taarifa katika kituo chochote
cha polisi ama ofisi za watendaji wa vijiji na kata pale watakapomuona
mtu au watu wanaowatilia shaka ili waweze kukamatwa na kuchunguzwa iwapo
walihusika na mauaji hayo.
Hivi karibuni Mkuu wa Wilaya ya Kahama,
Benson Mpesya alikiri kuwepo na wimbi kubwa la mauaji dhidi ya wanawake
na kusema mauaji yanayofanyika hivi sasa ni tofauti na yale ya awali
ambapo waliokuwa wakiuawa ni wanawake vikongwe wenye umri wa kuanzia
miaka 60.
Alisema, hivi sasa takwimu zinaonesha wanawake wanaouawa
ni pamoja na wale wenye umri wa kati ya miaka 50 hadi 20 ikiwemo
wanaochinjwa na waume au wenzi wao wa kiume kutokana na kinachodaiwa
kuwa ni wivu wa kimapenzi.
Mpesya aliyekuwa akihojiwa na mwandishi
wa habari aliyekuwa akifanya utafiti wa vitendo vya ukatili wa kijinsia
ikiwemo mauaji ya vikongwe katika wilaya hiyo ulioandaliwa na Chama cha
Wanahabari Wanawake nchini (TAMWA) alisema, takwimu zinaonesha hivi sasa
ndani ya mwezi mmoja hutokea mauaji ya wanawake wasiopungua watatu.
Alisema,
ugomvi wa kuwania mali ikiwemo mirathi na masuala ya kugombea ardhi ni
moja ya chanzo cha mauaji hayo ambapo hata hivyo katika kipindi cha
Novemba, mwaka jana wanawake watatu waliouawa kwa kuchinjwa akiwemo
mwanafunzi wa kidato cha nne chanzo kilikuwa ni wivu wa kimapenzi.
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment